JUHUDI ZA KIDIPLOMASIA ZASHIKA KASI BAADA YA KUUAWA KWA KIONGOZI WA HAMASI – MWANAHARAKATI MZALENDO

Marekani, Misri, na Qatar zimeungana katika juhudi za kidiplomasia ili kuzuia mivutano ya kikanda kuzidi kuwa mbaya baada ya kuuawa kwa kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh. Mataifa hayo matatu yamependekeza kuanzisha tena mazungumzo kati ya Israel na Hamas kuhusu kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka.

Kupitia taarifa ya pamoja, Marekani, Misri, na Qatar zilisema zimeandaa “mkataba wa mfumo” ambao unatoa muongozo wa utekelezaji, lakini bado unahitaji kukamilishwa. Mazungumzo hayo yamepangwa kufanyika tarehe 15 Agosti mjini Doha au Cairo, na Israel imethibitisha kuwa itatuma wapatanishi wake. Hata hivyo, Hamas haijatoa tamko lolote.

Mazungumzo haya yanakuja wakati ambapo hali ya wasiwasi imeongezeka, hasa baada ya Iran kuilaumu Israel kwa kuhusika na mauaji ya Haniyeh na kuapa kulipiza kisasi. Wakati Israel haijatoa maoni rasmi kuhusu mauaji hayo, hatua hizi za kidiplomasia zinaonekana kama jitihada za kupunguza hali ya taharuki ambayo inaweza kusababisha mgogoro mkubwa zaidi katika eneo hilo.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts