Bukoba. Zikiwa zimepita siku 52 tangu kukamatwa na kufunguliwa shtaka la tuhuma ya kumuua kwa kukusudia mtoto mwenye ualbino Asimwe Novath, washtakiwa wanaendelea kusota rumande baada ya kesi yao kupigwa kalenda tena leo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia namba 17740/2024, iliyoitwa leo Ijumaa Agosti 9,2024, kwa ajili ya kutajwa, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera huku wakiwa katika mwonekano tofauti
Washtakiwa hao ni Padri, Elpidius Rwegoshora na baba mzazi wa marehemu Novath Venanth, Nurdini Masudi, Ramadhani Selestine, Rweyangira Alphonce, Dastan Bruchard, Faswiu Athuman, Gozbert Alikad na Desdery Everigist.
Baada ya kufikishwa ndani ya chumba cha mahakama, Wakili wa Serikali, Erick Mabagala ameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kesi hiyo kutajwa kwa kile alichodai bado mchakato wa kuihamishia Mahakama Kuu haujakamilika.
“Kutokana na kutokamilika kwa taratibu za kuhamisha kesi hii kwenda Mahakama Kuu, tunaomba mtukufu hakimu mahakama yako iridhie kesi hii kuahirishwa ili itajwe tarehe nyingine tuone kama taratibu zitakuwa zimekamilika,” amesema Mabagala.
Kufuatia hoja hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Eliapokea Wilisoni ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 23,2024 litakapoitwa kwa ajili ya kutajwa.
“Kwa vile Mahakama hii haina mamlaka kisheria ya kusikiliza shauri hili na utaratibu wa kuihamishia katika mahakama yenye mamlaka ya kisheria ya kuisikiliza, haujakamilika, naiahirisha hadi Agosti 23,2024,” amesema hakimu, Wilsoni.
Tofauti na ilivyozoeleka kwa washtakiwa hao kujifunika usoni wanapofikishwa mahakamani hapo, leo mshtakiwa wa tatu, Nurdini Masudi ameibua maswali miongoni mwa watu waliofika kusikiliza shauri hilo baada ya kuonekana akiwa amevaa barakoa muda wote alipofika hadi kurejeshwa rumande huku akikohoa ‘mara kwa mara.’
Washtakiwa wengine wakati wanashushwa kwenye gari la polisi lenye rangi ya kijivu, wameonekana wakitembea kwa kuchechemea huku afya zao zikionekana kudhoofika tofauti na siku walipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 28, mwaka huu.
Huku akionekana kulengwa na machozi, mshtakiwa namba moja katika shauri hilo Padri, Rwegoshora alikuwa amevalia sweta zito jeusi huku akıwa amenyolewa nywele zote kichwani na kuachiwa ‘kipara’ kilichong’aa juani.
Kwa upande wa baba wa marehemu, Novath Venanth, ambaye mara zote amekuwa akiinamisha kichwa chini awapo mahakamani ili kutoonekana, leo alionekana mwenye kujiamini wakati wote huku akizitazama kamera za waandishi wa habari bila hofu.
Washtakiwa nane kati yao hawana wakili wa kuwatetea, kasoro Padri Rwegoshora anayewakilishwa na wakili wa Kujitegemea, Mathias Rweyemamu ambaye hata hivyo leo hakuonekana mahakamani hapo wakati kesi hiyo ikitajwa.