Kete ya Mwisho ya medali kwa Tanzania Olimpiki 2024

Kama sio Alphonce Simbu ni Gabriel Geay ambao kesho Agosti 10 watakuwa katikati ya miamba ya dunia ya mbio ndefu kusaka medali ya Olimpiki msimu huu.

Nyota hao wa mbio ndefu nchini ndiyo tegemeo kubwa la medali kwa timu ya Tanzania ambayo kesho Jumamosi itakuwa barabarani ikichuana na magwiji wengine wa dunia huku ‘dada’ zao, Jackline Sakilu na Magdalena Shauri wakifunga hesabu Keshokutwa Jumapili upande wa wanawake.

Nyota hao wako mjini Paris Ufaransa tangu Agosti 7 wakiwa na kocha wao, Anthony Mwingereza, tayari kwa mbio hiyo itakayowashindanisha na nyota bora wa muda wote wa masafa marefu duniani, mhabeshi Kenenisa Bekele na Mkenya Eliud Kipchoge.

Simbu atachuana na Kipchoge kwa mara nyingine kwenye Olimpiki ya Paris baada ya ile ya Rio 2016 nchini Brazil alipokwenda naye sambamba na kuachwa mwishoni na Mkenya huyo aliyekuwa bingwa na Simbu kumaliza kwenye tano bora.

Akizungumza na Mwananchi, Simbu amesema nafasi ya medali kwa Tanzania msimu huu ipo, akiahidi mojawapo itakuwa ni yake, akitaka kuandika rekodi nyingine baada ya ile ya 1980 Tanzania ilipotwaa medali mbili za fedha kwenye Olimpiki ya Moscow, Russia.

Nahodha huyo wa Tanzania mwenye medali ya shaba ya dunia na ya fedha ya Jumuiya ya Madola anataka kuandika rekodi kwenye Olimpiki, japo hajasema ni medali gani kati ya dhahabu, fedha au shaba anaitaka kwenye Olimpiki hiyo.

Simbu atakayewaongoza wenzake katika kete hiyo ya mwisho kwa Tanzania amesema hawatarajii kurudi mikono mitupu msimu huu.

“Nafahamu upinzani ni mkali,  huku kuna Kipchoge, kule Bekele na wengine waliopo, bahati nzuri wengi wao tunafahamiana, tumekimbia nao mara nyingi hivyo Olimpiki hii moto utawaka, medali kwa Tanzania ni lazima,” amesema.

Simbu kwa mara ya kwanza atakimbia sambamba na Geay  Mtanzania anayeshikilia rekodi ya taifa ya marathoni ambaye licha ya kutoka kwenye majeruhi ya kifundo cha mguu, amesisitiza yuko fiti kwa ushindani na tegemeo ni kufanya vizuri.

Kocha wa Tanzania, Anthony Mwingereza amesema kazi yake imekwisha, jukumu lililobaki ni kwa wanariadha hao kutumia saa mbili za mbio hizo kiushindani.

“Sina shaka na medali, nyota wangu wamejiandaa na wote wana uzoefu wa mashindano makubwa, kikubwa ni kuwaombea waamke salama na wawe fiti, wako vizuri wana pumzi, kasi na mbinu za kutosha kukabiliana na upinzani.

Hata hivyo licha ya Kipchoge na Bekele ambao wamekutana Paris kwa mara nyingine tena tangu walipokuta mwaka 2003 kwenye mashindano ya Dunia ikiwa ni zaidi ya miongo miwili, Mkenya akichukua dhahabu ya mita 5000 na Mhabeshi shaba kuwa ndiyo wanariadha wa marathoni  wanaotajwa zaidi kwenye ushindani wa Jumamosi,  Simbu amesisitiza medali ya Tanzania ipo.

“Tuna medali yetu kwenye marathoni hii, siwezi kusema ni ya kwanza, ya pili au ya tatu, lakini ipo,” amesitiza Simbu.

Kipchoge ( 37) anafukuzia taji la tatu mfululizo la marathoni kwenye Olimpiki huku Bekele (42) ambaye ni miongoni mwa wakongwe kwenye mbio hiyo sanjari na Mhabeshi mwenzake ambaye sasa mwanariadha wa Uswizi, Tadesse Abraham akiwa anapambana kuandika rekodi ya marathoni ya Olimpiki.

Bekele ana rekodi ya medali tatu za dhahabu za Olimpiki kwenye mbio ya  mita 5000 na ​​10,000 akisaka mafanikio hayo  kwenye marathoni.

Mwaka 2019 alijaribu bila mafanikio  kushusha rekodi ya Kipchoge kwa saa 2:01:41 mjini Berlin, muda unaomfanya kuwa mwanariadha wa tatu mwenye kasi zaidi kwa ]]muda wote nyuma ya Kipchoge na Kelvin Kiptum aliyefariki kwa ajali ya gari.

Nyota wengine wanaotajwa kwenye ushindani Jumamosi ni Mhabeshi, Alexander Munyao bingwa wa London marathon mwenye rekodi ya medali za dunia mara tano,  Deresa Geleta, mshindi wa Marathon ya Seville, na bingwa wa dunia wa 2022, Tamirat Tola.

Wengine ni bingwa wa dunia kutoa Uganda, Victor Kiplangat, Mholanzi mwenye medali ya fedha ya Tokyo marathoni 2020,  Abdi Nageeye na mshindi wa medali ya shaba wa Ubelgiji, Bashir Abdi.

Related Posts