KUMNUNULIA HELIKOPTA RAIS NI KUJIPENDEKEZA – MWANAHARAKATI MZALENDO

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA katika mkoa wa kichama wa Ilala, Dedan Wagwe, amekosoa vikali kitendo cha kumnunulia Rais helikopta kwa ajili ya kampeni zake binafsi, akielezea hatua hiyo kama mfano wa kujipendekeza. Akizungumza katika kipindi cha #SupaBreakfast, Wagwe alisema kwamba kitendo hicho ni sawa na utamaduni unaozidi kushamiri wa watu kujitolea kumnunulia Rais fomu za kugombea, hatua aliyoitafsiri kama harakati za kutafuta umaarufu wa kibinafsi.

“Hii ni sawa na mtindo wa kawaida ambao nautafsiri kama kujipendekeza, kama wale wengine wanao mnunulia Rais fomu,” alisema Wagwe.

Kauli ya Wagwe imeibua mjadala kuhusu namna viongozi wanavyojihusisha na kampeni za kisiasa, na inachochea mjadala mkubwa kuhusu ushawishi wa fedha katika siasa za Tanzania. Katika mazingira ambayo nafasi za kisiasa zinaonekana kuwa na mvuto mkubwa kwa wafanyabiashara na watu wenye uwezo mkubwa kifedha, baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa hatua kama hizi zinaweza kupunguza uwazi na usawa katika mchakato wa kisiasa.

Wagwe ametoa wito kwa vijana na wafuasi wa chama chake kuwa macho na kuelewa madhara ya hatua kama hizi, akisisitiza umuhimu wa siasa zenye misingi ya maadili na uwajibikaji badala ya kutegemea zawadi au msaada wa kifedha kutoka kwa watu binafsi.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts