Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza wasiwasi wake kuhusu baadhi ya mapendekezo kwenye muswada wa marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji, ambao unalenga kutoa hadhi maalumu kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi wenye uraia wa mataifa mengine (Diaspora).
LHRC imeainisha changamoto kadhaa zinazoweza kujitokeza kutokana na vifungu vya muswada huo, ikiwemo mamlaka makubwa aliyopewa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na uwezekano wa kigezo cha “maadili mema” kutumika kwa upendeleo au ubaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, leo Agosti 9, 2024 , amebainisha kwamba kuna hatari ya matumizi ya vigezo visivyo wazi katika kutoa hadhi maalumu kwa Watanzania hao.
LHRC inapendekeza kwamba mamlaka ya kufuta hadhi maalumu iondolewe kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na kupewa Mahakama ili kuhakikisha maamuzi yanafanywa kwa uwazi na kufuata sheria.
Henga amesisitiza kwamba muswada huo unahitaji marekebisho zaidi, hasa kwenye vipengele vinavyompa Kamishna Mkuu mamlaka ya pekee.
Aidha, amependekeza kuondolewa kwa sharti la kumiliki kampuni kwa kushirikiana na raia wazawa, akisema sharti hilo linapunguza maana ya hadhi maalumu kwa watu wenye asili ya Tanzania.
Pia, Henga ameeleza wasiwasi wake kuhusu kifungu kipya kinachopendekeza mamlaka ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji kutoa hadhi maalumu kwa mtu yeyote kwa kuzingatia mazingira maalumu, ikiwa mtu huyo ana kipaji au ujuzi wa pekee. Ameonya kuwa kumnyima mtu hadhi maalumu kwa msingi wa tathmini ya maadili kunaweza kupelekea ubaguzi, kinyume na Ibara ya 13 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.
Mapendekezo ya LHRC yanakuja baada ya mjadala wa muda mrefu kuhusu uraia pacha, ambapo Watanzania wengi wanaoishi nje walikumbana na changamoto za kisheria katika nchi wanazoishi, ambazo haziruhusu uraia pacha.
Hadi sasa, hadhi maalumu imeonekana kama suluhisho la muda kwa Watanzania wa diaspora, ili waweze kudumisha uhusiano na nchi yao ya asili bila kupoteza haki zao za uraia katika nchi walizoamua kuishi.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, alieleza bungeni kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha utoaji wa hadhi maalumu kwa diaspora, hatua ambayo inatarajiwa kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania wanaoishi nje ya nchi.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.