Mafanikio hayo ya M23 yanayozua wasiwasi yanatokea licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyopo, na yamezua hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Wakati huo huo, huko Kinshasa, mahakama ya kijeshiimetoa adhabu kali dhidi ya waasi, lakini je, itatosha kuzuia kusonga kwao mbele?
Vijiji zaidi ya mia vinadhibitiwa na M23
Hali katika eneo la Rutshuru, mkoa wa Kivu Kaskazini, imekuwa ya hatari. Kwa mujibu wa ripoti ya kundi la harakati za kiraia la Lutte pour le changement (LUCHA), karibu eneo zima sasa liko mikononi mwa waasi wa M23, wanaosaidiwa na Rwanda.
Kulingana na Lucha, vijiji na makazi 101 sasa viko chini ya udhibiti wa waasi, ikiwemo mji wa kimkakati wa Nyakakoma kwenye Ziwa Edward.
Stewart Muhindo, mwanaharakati wa Lucha, anasema, “Ripoti yetu kuhusu mafanikio ya M23 ina malengo mawili. Kwanza ni kukumbusha kwamba maeneo haya, ingawa yamekaliwa, bado ni sehemu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa sababu tunajua kwamba nyuma ya vita hivi kuna wazo la kutenganisha baadhi ya maeneo kutoka DRC,” alisema Muhindo. “Makazi 101 tayari yanadhibitiwa na wageni, ni mengi sana. Tunataka pia kuhimiza mamlaka za Kongo kurejesha maeneo haya.”
Hukumu hazitoshi kuwazuia waasi
Alhamis, mahakama ya kijeshi huko Kinshasa iliwahukumu kifo watu 26 kwa kuhusika kwao katika uasi wa M23. Miongoni mwa waliohukumiwa bila kuwepo ni Corneille Nangaa, aliyekuwa rais wa Tume Huru ya Uchaguzi, na kwa sasa kiongozi wa kundi la uasi la AFC.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mwenyekiti wa shirika la kiraia la Bwito, Kambale Lupasula, hukumu hizi hazitoshi kuzuia maendeleo ya waasi, serikali inapaswa kuchukua hatua.
“Waasi wanaendelea kusonga mbele. Sasa wamefika hadi Nyakakoma. Kwa kuwa wamefika Nyakakoma, sisi kama wawakilishi wa asasi za kiraia tumejawa na hofu,” alisema Lupasula. “Nyakakoma inatoa njia ya moja kwa moja kuingia Beni-Kyavinyonge. Hamuwezi kuona kwamba hali inazidi kuwa mbaya? Licha ya yote haya, rais bado anaendelea kuzingatia hukumu. Hii itatupeleka wapi?”
Wakati waasi wakiendelea kupiga hatua, watu wa Rutshuru na maeneo jirani wanaishi katika hofu ya kudumu.