Moshi. Mahakama Kuu imewaidhinisha wananchi 10 kuwawakilisha wenzao 318 katika shauri la madai dhidi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Kampuni ya Uendeshaji Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO).
Kwa zaidi ya miaka 20 sasa, kumekuwapo mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wanaoishi vijiji vinavyozunguka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na uwanja huo, wakiituhumu KIA na KADCO kuwapora maeneo yao ya asili.
Sheria inataka kufunguliwa kesi ya uwakilishi pale wadai wanapokuwa wengi, hivyo wananchi hao walifungua maombi namba 13361 ya mwaka 2024 kuomba Mahakama Kuu iwaidhinishe wawakilishi wao 10.
Maombi hayo yalifunguliwa na Issa Mgala, Kimangano Mdee, Athman Mwanga, Said Ndoile, Abjadi Mkwizu, Paul Magwero, Ramadhan Juma, Adam Mahanyi, Beatrice Msofe na Machaku Mdee dhidi ya TAA kama mjibu maombi wa kwanza.
Katika maombi hayo, waliwaunganisha KADCO kama mjibu maombi wa pili, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kama mjibu maombi wa tatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa nne.
Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi aliyesikiliza maombi hayo, ameyakubali kupitia uamuzi wake wa Agosti 7, 2024, uliowekwa Agosti 9, 2024 katika tovuti ya Mahakama.
Msingi wa maombi hayo uliopatikana katika viapo vya pamoja vya waombaji, ni kwamba wananchi hao 328 wanakusudia kuwafungulia shauri la madai wajibu maombi hao wanne kwa kuingia kwa jinai katika ardhi yao.
Kulingana na uchambuzi wa Jaji Kilimi, waombaji hao walieleza wamejaribu kutaka suluhu ya mgogoro huo kwa njia ya amani na pasipo mafanikio na kwamba, ushahidi watakaouwasilisha unafanana kwa waombaji wote 328.
“Kwa vile idadi ya waombaji ni kubwa, walikutana katika kikao kilichofanyika Machi 10, 2024 na kwa mafanikio waliwateua waombaji hao 10 kuwawakilisha wenzao 318 katika shauri la ardhi wanalokusudia kufungua,” amesema Jaji Kilimi.
Wakati maombi hayo yalipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa, wakili Francisca Lenguju alijitokeza kuwawakilisha waombaji, huku mawakili wa Serikali, Gloria Isangya na Dommy Rimoy wakiwatetea wajibu maombi.
Wakili Francisca aliiambia mahakama kuwa waombaji walikuwa hawajapatiwa kiapo kinzani lakini Wakili Glorian alieleza kuwa wajibu maombi hawakusudii kuwasilisha kiapo kinzani kwa kuwa hawapingi maombi hayo.
Jaji Kilimi alisema baada ya kupitia hoja hizo na hasa ikizingatiwa kuwa wajibu maombi hawapingi maombi hayo, hoja ni kama maombi hayo yamekidhi matakwa ya kisheria kuiwezesha Mahakama kutoa kibali hicho cha uwakilishi.
Kwa mujibu wa Jaji, msimamo wa kisheria unataka waombaji wajenge msingi kuwa watu wanaotaka kuwawakilisha katika shauri wana masilahi sawa ya kuwafungulia mashtaka walengwa na wako radhi kujiunga kwa hiari katika kesi.
Akirejea viapo vya waombaji hao 10, Jaji alisema ni wazi waombaji hao 10 wanakusudia kuwawakilisha wenzao 318 kupinga hatua ya wajibu maombi kuingia kwa jinai katika ardhi yao na katika orodha zipo saini za wananchi wote 328.
Jaji alisema mahakama imeridhika maombi hayo yapo kisheria mbele ya mahakama, hivyo waombaji wamepewa kibali cha kuwawakilisha wenzao na kuwataka kufungua kesi hiyo ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwa uamuzi huo.
Iwapo wananchi hao watafungua shauri hilo kama walivyoruhusiwa na mahakama, litakuwa shauri la pili kufunguliwa baada ya Februari 2024, Mahakama Kuu kuyakataa maombi ya wananchi wa vijiji vinane kuhusu mgogoro huohuo.
Wananchi hao walifungua maombi hayo namba 2 ya mwaka 2024 wakipinga amri ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kutangaza eneo lenye ukubwa wa hekta 11,000 kuwa mali ya Serikali kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA).
Wananchi hao kutoka vijiji vya wilaya za Meru mkoani Arusha na Hai mkoani Kilimanjaro, walifungua maombi hayo dhidi ya RC kwa cheo chake kama mdaiwa wa kwanza, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama mdaiwa wa pili.
Walikuwa wanadai agizo hilo la RC alilolitoa Novemba 2, 2022 lilikuwa kinyume cha sheria, lisilo na mantiki, lisilo na sababu na linakiuka haki ya asili inayotoa haki ya kusikilizwa na kwamba lilikiuka kanuni na taratibu za nchi.
Mbali na ombi hilo, walikuwa wanaiomba mahakama itoe amri dhidi ya RC ya kumzuia kuwaondoa kwa nguvu, kutowabugudhi na kuwatisha waombaji kutoka vijiji hivyo vinane, pia mahakama iwape nafuu yoyote kadri itakavyoona inafaa.
Hata hivyo, Jaji Kilimi alisema amepakuwa na kusikiliza video ambayo iliwasilishwa kortini kama kielelezo kuthibitisha kauli ya RC, lakini hajaona mahali ambako RC alitoa amri ya kuwaondoa wadai katika ardhi hiyo.
Kilichomo ni kuwa RC aliwajulisha tu wananchi waliohudhuria katika mkutano wa hadharani kuwa Serikali inafanya uhakiki wa mipaka ya KIA na atakayekuwa ndani ya eneo la KIA masilahi yake yangelindwa kabla ya kuondolewa.
Jaji aliasema kile kilichosemwa katika mkutano huo ni kuwa RC alikuwa anatumia mamlaka yake kama mlinzi wa amani na alikuwa na wajibu huo wa kuwafanya wananchi wawe na ufahamu kwa jambo lolote ambalo Serikali inafanya.
“Madai ya waombaji kuwa Novemba 9, 2022 kazi ya uwekaji vigingi ilianza naona siyo haki kuhusu nani anawajibika, kwa sababu hakuna uthibitisho kama walioweka vigingi walitumwa na RC au kamishina wa ardhi,” alisema Jaji Kilimi.
Kutokana na maelezo hayo, Jaji Kilimi alisema ameridhika maombi ya wananchi hao hayakukidhi masharti ya kupewa amri ya kubatilisha agizo lililodaiwa ni la RC, hivyo linatupwa na kwa asili ya shauri hilo, kila upande utabeba gharama zake.