Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu Klabu ya Dar es Salaam Young Africans Sports kufanya mapitio ya marejeo ya shauri la madai namba 187/2022 lililofunguliwa na Juma Magoma na mwenzake Geofrey Mwaipopo.
Pia mahakama hiyo imetupilia mbali mwenendo mzima wa kesi hiyo ya madai namba 187/2022 na kuweka kando amri zote zilizotolewa katika hukumu iliyotolewa Agosti 2, 2023.
Pia, Mahakama hiyo imeamuru Magoma, Mwaipopo na Abeid Mohamed Abeid, wailipe
Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga, gharama za shauri hilo la mapitio.
Uamuzi huo umetolewa leo, Agosti 9, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga, wakati akitoa uamuzi wa shauri la maombi ya marejeo ya uamuzi uliobatilisha Katiba ya Yanga, maarufu kama Katiba ya Yanga ya mwaka 2011.
Katika shauri hilo Klabu ya Yanga kupitia wakili wake, Kalaghe Rashid na Respocius Didas waliiomba mahakama hiyo irejee uamuzi uliobatilisha Katiba yake ya mwaka 2011.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Pamela Mazengo, Agosti 2, 2023 ilibatilisha Katiba ya sasa ya Yanga ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2011.
Uamuzi huo ulitokana na kesi iliyofunguliwa Agosti 4, 2022 na Magoma na mwenzake Mwaipopo, wanaojitambulisha kama wanachama wa klabu hiyo.
Katika kesi hiyo Magoma na Mwaipopo walipinga Katiba hiyo ya mwaka 2011 kuwa si halali kisheria na kwamba Katiba halali inayotambulika ni ile ya mwaka 1988.