Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema teknolojia ya uzalishaji wa malisho aina ya Juncao iliyoanza kutumika nchini, ni suluhisho la kumaliza changamoto za malisho ya mifugo inayowakabili wafugaji kwa nyakati tofauti.
Nyasi za Juncao zenye asili ya China zinaweza kutumiwa pia kuzalisha uyoga unaoweza kutumiwa pia kama chakula cha wanyama, mbolea, mafuta ya majani na nyenzo ya bidhaa za mafuta yanayokuwa katika ubora wa hali ya juu katika mazingira rafiki.
Waziri Ulega ameeleza hayo leo Ijumaa Agosti 9, 2024 alipotembelea shamba la Serikali la mbegu za malisho ya Juncao lililopo Vikuge, Kibaha mkoani Pwani.
Katika ziara hiyo, Ulega aliambatana na ugeni kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) waliowakilishwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Earle Courtenay Rattray waliokwenda kujionea maendeleo ya teknolojia hiyo.
Waziri Ulega, amesema uwepo wa malisho yanayotokana na Juncao utawezesha kupunguza migogoro kati ya wafugaji na wakulima, huku akisema katika shamba hilo wamepanda majani ya Juncao ekari 21 kuanzia mwaka 2021 hadi 2024.
“Mbegu zilizozalishwa ni kilo 178,262, huku zaidi ya wakulima 957 wakishiriki kulima majani ya Juncao kwa hatua tofauti tofauti.
“Juncao ni sehemu katika programu ya tutunzane ‘Mvomero’ iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan inayolenga kuhamasisha wafugaji kulima malisho katika maeneo yao, kuhifadhi mazingira na kupunguza migogoro kati yao na wakulima,” amesema Waziri Ulega
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega ameushukuru Umoja wa Mataifa kwa mchango wake wa kuwajengea uwezo wataalamu mbalimbali katika wizara yake ikiwemo kuifahamu vema teknolojia hiyo ya ulimaji majani ya Juncao.
“Teknolojia hii tumeichukua kama ni suluhu ya mahitaji ya malisho katika Taifa letu,” amesisitiza Waziri Ulega.
Naye, Balozi Rattray ameelezea kufurahishwa na maendeleo ya Juncao, akimpongeza Rais Samia kwa kuonesha utayari wa kuipokea teknolojia hiyo inayotarajiwa kuwa moja ya masuluhisho ya changamoto ya malisho na migogoro ya wakulima na wafugaji.