Hadi sasa Rahimi anaongoza kama mfungaji bora kwa kupachika mabao manane, wakati kukitarajiwa fainali kati ya Uhispania na bingwa wa mwaka 1984 wa Olimpiki, mwenyeji Ufaransa, siku ya Ijumaa (Agosti 9).
Kwenye mchezo wa hoki, Uholanzi iliibwaga Ujerumani 2-1 na hivyo kuibuka na medali ya dhahabu, ikiwa ni ya kwanza kwa timu yake ya wanaume zangu mwaka 2000 na ya tatu kwenye historia ya taifa hilo la Ulaya ya Kati. India pia iliibwaga Uhispania 2-1.
Kwenye mbio za baiskeli, Benjamin Thomas aliipatia Ufaransa medali yake ya 14 ya dhahabu kwenye michezo ya mwaka huu ya Olimpiki.
Soma zaidi: Bondia Khelif aomba kukomeshwa uonevu dhidi ya wanamichezo
Ufaransa ilifanya vyema pia kwenye mchezo wa mpira wa vikapu, ambapo nyota wake, Victor Wembanyama aliekea kutimiza ndoto yake ya kutwaa medali ya kwanza ya dhahabu baada ya kumsaidia Les Bleus kuibwaga Ujerumani na kujiweka nafasi ya kucheza na Marekani, ambayo iliibwaga Serbia kwa vikapu 95 kwa 91.
Ufaransa iliichabanga Ujerumani vikapu 73 kwa 69.
Wembanyama, mwenye umri wa miaka 20 hakucheza michezo ya mwisho ya Olimpikimiaka mitatu iliyopita mjini Tokyo, wakati Ufaransa iliposhindwa na Marekani. Wababe hao wawili watakumbana tena kesho Jumamosi.
Marekani yaongoza kuzowa medali
Kufika sasa, siku tatu kabla ya Michezo ya Olimpiki kumalizika, Marekani ndiyo inayoongoza kwa kutwaa medali nyingi zaidi, kwani ina medali 30 za dhahabu kati ya medali 103 ilizokusanya.
Kwa upande wake, China ilipata medali yake ya sita ya dhahabu hapo jana baada ya mpigambizi wake Xie Siyi kushinda kwa kuzamia mita tatu majini.
Soma zaidi: Uganda yashinda medali nyingine ya fedha ya Olimpiki
Indonesia kwa upande wake ilipata medali ya dhahabu kupitia mchezo wa kukwea juu iliyoletwa na Veddriq Leonardo.
Kwenye mpira wa wavu upande wa wanawake, Kanada na Brazil zilisonga mbele kuwania medali za dhahabu, huku upande wa wanaume ukiwakutanisha Wajerumani na Waswidi.
Marekani, ambayo ilikuwa bingwa mtetezi upande wa wanawake, ilishang’olewa kwenye hatua ya robo fainali, na sasa Kanada inajipanga kwa medali yake ya kwanza kwenye fainali baada ya kuibwaga Uswisi.
Brazil ilipambana na kuiangusha Australia na sasa inasaka medali yake ya kwanza ya dhahabu tangu mwaka 1996.