MACHOZI yake baada ya mechi iliyowatupa Ureno nje michuano ya Euro pale Ujerumani yalikuwa machozi ya mwisho katika soka. Hatujua. Labda alilia zaidi kwa sababu alijua ilikuwa mechi yake ya mwisho katika soka. Pepe. Mreno kichaa. Mreno jeuri.
Aliwahi kuandika Ben Mtobwa. ‘Machozi ndio njia pekee imalizayo huzuni ya mwanamke’. Hapana. Alikosea. Hata wanaume wanatoa. Hata wahuni wanatoa machozi. Pepe ni mmojawapo. Alilia siku ile. Wengi hatukujua kilichokuwa kimejificha nyuma yake.
Juzi alitangaza rasmi kuachana na soka. Jumla. Februari 26 mwaka huu alitimiza miaka 41. Hakuna unachoweza kufanya zaidi ya kumsifu Pepe. Sio wachezaji wengi wanaotimiza miaka 41 wakicheza soka katika kiwango cha juu katika nafasi yake. Kucheza Euro katika umri huo hakikuwa kitu cha kawaida sana.
Nakukumbusha tu, Pepe ni mkubwa kuliko baba yake Lamine Yamal. Ina maana Pepe alianza kucheza na watoto wake. Umri wake ni rahisi kwa kipa kufika huko. Kipa eneo lake analokimbia uwanjani ni dogo. Ni rahisi kucheza kwa muda mrefu. Lakini kuna washambuliaji wanaofika katika umri huo huku wakicheza katika kiwango cha juu.
Kuna washambuliaji ambao kazi yao ni kuvizia katika boksi. Wanajikuta wanakimbia katika eneo dogo tu. Kuna wachezaji pia ambao baadaye wanabadili nafasi au staili zao za uchezaji na kuwa waviziaji kwa ajili ya kudumisha urefu wao katika maisha yao ya soka.
Mfano ni rafiki mkubwa wa Pepe, yaani Ronaldo. Wakati akiwa kinda kisha akakomaa alikuwa bingwa wa mbio na chenga. Umri ulipomkamata akaamua kukaa katika boksi na kuvizia. Ni kweli kwa sasa amechoka lakini hadi sasa hivi anacheza soka. Ni katika umri wa miaka 38. Februari anatimiza miaka 39. Lazima umsifu.
Hata hivyo, baada ya kila kitu hatimaye Pepe ameamua kunyoosha mikono juu. Wakati namtazama Euro nilidhani angeweza kustaafu kucheza timu ya taifa tu, lakini kumbe alikuwa ameamua kustaafu mazima. Ameamua kutundika daluga juu kama mchezaji wa kulipwa. Pepe amenikumbusha mengi.
Kitu cha kwanza? Amenikumbusha kuwa miongoni mwa wanasoka waliohama mataifa yao kucheza taifa jingine kwa sababu mbalimbali. Siku hizi imekuwa kawaida, lakini wakati Pepe anatangaza kucheza Ureno na sio Brazil alikozaliwa halikuwa jambo la kawaida sana. Achana na wale ambao walizaliwa eneo fulani huku wazazi wao wakitoka nchi fulani.
Pepe hakuzaliwa Ureno. Alizaliwa Brazil na halihama utaifa wake kwa ajili ya kucheza Ureno akiwa na umri wa miaka 24. Nadhani alisubiri sana kucheza timu ya taifa ya Brazil. Alipoona nafasi ni ndogo akaamua kucheza Ureno ambako aliona nafasi ni kubwa. Ilitokea kwake na kwa Diego Costa. Pepe hakucheza timu ya vijana ya Brazil wala Ureno.
Jaribu kufikiria namna ambavyo Lionel Messi alikwenda Hispania akiwa na miaka 13, lakini baadaye aliamua kucheza kikosi cha vijana cha Argentina na kisha baadaye kikosi cha wakubwa. Pepe aliamua kusubiri. Hakwenda Brazil wala Ureno. Kwa sasa imeanza kuwa mazoea, lakini Pepe alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo mwanzo kabisa.
Lakini baada ya kila kitu tunaweza kuanza kujiuliza. Pepe ni kizazi cha mwisho cha wachezaji masela? Ndio, nyakati ngumu hazipiti lakini watu wagumu wanapita. Hata hivyo, siku hizi tuna namna tofauti ya kuzikabili nyakati ngumu. Kuna wachezaji wagumu wanaoweza kuzikabili nyakati ngumu katika namna ya ulaini.
Pepe alikuwa ni mchezaji mgumu, mhuni, mkorofi uwanjani. Kadi za njano na nyekundu zilikuwa kitu cha kawaida kwake. Yeye pamoja na rafiki yake Sergio Ramos wanaweza kuwa kizazi cha mwisho mwisho cha wachezaji wa aina hii. Wachezaji masela uwanjani. Na hasa zaidi katika nafasi zao.
Katika nafasi mbalimbali wachezaji wa namna hii wametoweka. Pale katika kiungo waliwahi kuwepo kina Roy Keane, Patrick Vieira, Javier Mascherano, Steffan Efenberg na wengineo kibao. Lakini leo tuna viungo mafundi wa kawaida tu. Usela umeondoka katikati ya uwanja. Na hata ile nafasi iliyokuwa inaitwa kiungo wa ulinzi (defensive midfielder) imeondoka na badala yake kuna kiungo muunganishaji (holding midfielder).
Leo tuna kina Rodri, Thomas Partey na wachache wengineo. Sio masela. Hakuna uhuni katikati ya uwanja. Hata eneo la mbele wakorofi wameondoka. Wa mwisho mwisho walikuwa hawa kina Zlatan Ibrahimovic. Sasa hivi tuna watu wana futi kadhaa hewani lakini sio wababe. Mfano ni kama Erling Haaland au Roberto Lewandowski. Hawana ubabe sana zaidi ya kuzingatia soka.
Nadhani mpira umetawala zaidi kuliko ubabe. Huku katika ulinzi nadhani kina Pepe ndio wanamalizia. Rafiki yake, Sergio Ramos hadi leo hajatutangazia timu mpya baada ya kuachana na Sevilla mwishoni mwa msimu uliopita. Hatujui kama ataenda Saudi Arabia au Marekani au atatangaza kustaafu soka.
Sasa sio tu kwamba mabeki wababe wanaondoka lakini ubabe wa siku hizi unapaswa uendane na mambo mengi. Uendane na kujua mpira zaidi. Akina Pep Guardiola wanatuambia mlinzi lazima awe na ubora mwingi wa kucheza soka kuanzia nyuma. Sasa hivi mabeki wa kati wanacheza kama viungo. Nao wanapaswa kutuliza mpira na kucheza kuanzia nyuma. Wakati mwingine wanakuwa na pasi nyingi kuliko viungo.
Rafiki zangu kina Sol Campbell sijui kama wangeweza kucheza mpira wa kileo. Zamani mabeki kazi yao kubwa ilikuwa kukaba zaidi na kuondosha mpira katika hatari. Hata Pepe ni mmoja kati ya wachezaji wa aina hii. Ndio maana najiuliza kama ni vizazi vya mwisho vya wachezaji wahuni ambavyo vinatoweka.
Akapumzike kwa amani Pepe. Kuna mahala nilikuwa nabishana na watu kama Pepe atakumbukwa kuwa miongoni mwa mabeki bora kuwahi kutokea ulimwenguni. Binafsi siamini hilo. Kwamba kwa ubora akae daraja moja na kina Paolo Maldini, Rio Ferdinand, Franco Baresi, Virgil Van Dijik, Ronald Koeman na wengineo, hapana.
Atakumbukwa tu kwa kuwa beki wa kazi chafu. Beki ambaye angefanya kila kitu kwa ajili ya kulihami lango. Angemrukia mtu mguu wa shingo na mengineyo. Mabeki wa kazi. Sidhani kama alikuwa na kipaji kikubwa. Hapana. Alikuwa beki aliyezaliwa na kukulia ghetto.