Unguja. Bei ya petroli imeshuka, huku dizeli ikipanda kwa asilimia 6.02 kisiwani Zanzibar.
Bei ya petroli imeshuka kutoka Sh3,085 kwa lita moja hadi Sh3,062 ikiwa ni tofauti ya Sh23 sawa na asilimia 0.75.
Dizeli kwa Agosti itauzwa kwa Sh3,259 kutoka Sh3,074 ikiwa kuna tofauti ya Sh185 sawa na asilimia 6.02. Bei hizo zimeanza kutumika leo Agosti 9, 2024.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura) mafuta ya ndege yatauzwa Sh2,843 ikilinganishwa na Sh2,809 Julai, ikiwa ni tofauti ya Sh34, huku mafuta ya taa yakibakia bei ileile ya Sh3,200 kwa lita.
Akitangaza bei hizo leo Agosti 9, 2024, Ofisa Uhusiano wa Zura, Mbaraka Haji, ametaja sababu za kupungua na kuongezeka kwa bei hizo ni kutokana na gharama za mafuta katika soko la dunia, gharama za uingizaji wa mafuta na mabadiliko ya fedha za kigeni.
“Sababu nyingine ni gharama za usafiri, bima na premium hadi Zanzibar, kodi na tozo za Serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja,” amesema.
Kwa sasa Zanzibar inapokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga na kuyahifadhi katika bohari ya Maruhubi iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi.Bohari hiyo ina uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 21.
Wakati bohari hiyo ikiwa na uwezo huo, matumizi ya mafuta Zanzibar ni kati ya lita za ujazo milioni 30 hadi 40 kwa mwezi, huku Zanzibar ikiwa na vituo vya mafuta zaidi ya 100.
Baadhi ya watumiaji wa nishati hiyo wamesema punguzo hilo siyo dogo, lakini ni vyema kukawa na mipango madhubuti ya kuwa na vituo vya kuhifadhi mafuta mengi.
“Tukiwa na mafuta angalau ya miezi sita itapunguza hili la bei kuwa inabadilika kila mara kwani watu watahifadhi na pindi bei zitakapokuwa zinabadilika kwenye soko la dunia huku tunaendelea kuwa na ziada,” amesema Shaib Hussein Mwalim, mkazi wa Kikwajuni.