Dar es Salaam. Watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kuhusika na tukio la kumbaka na kumlawiti binti mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.
Video za tukio hilo zilisambazwa Agosti 4, 2024 kwenye mitandao ya kijamii, zikionyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo, kwa kile walichodai ametembea na mume wa mtu waliyemwita kwa jina la ‘Afande’.
“Uchunguzi uliofanyika hadi sasa umefanikisha kumpata binti aliyefanyiwa ukatili huo na amehifadhiwa eneo salama na anaendelea kupata huduma zinazostahili kupewa mtu aliyefanyiwa ukatili wa aina hiyo. Aidha, uchunguzi umebaini tukio hilo lilifanyikia eneo la Swaswa katika Jiji la Dodoma Mei 2024,” imesema taarifa ya jeshi hilo na kuongeza:
“Pia hadi sasa uchunguzi umefanikisha kukamatwa watuhumiwa wanne kati ya sita ambao walipanga na kutekeleza uhalifu huo. Watuhumiwa hao wamekamatwa mkoani Dodoma na Mkoa wa Pwani ambao ni Clinton Honest Damas kwa jina maarufu Nyundo, Praygod Edwin Mushi, Amini Lord Lema na Nikson ldala Jakson.”
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Agosti 9, 2024 na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Aidha, Polisi wamesema wamewakamata watuhumiwa wanne jijini Dar es Salaam kwa kosa la kusambaza picha mjongeo za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii, ambao ni Flora Mlombola, Aghatha Mchome, Madatha Jeremiah Budodi na James Nyanda Paulo.
Endelea kufuatilia Mwananchi.