BAADA ya kuukosa ubingwa wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mwanza msimu uliopita, Profile imekuja kivingine msimu huu baada ya kuanza kwa ushindi dhidi ya bingwa mtetezi, Eagles na kulipa kisasi cha kufungwa kwenye fainali ya msimu uliopita.
Profile ambayo ni mabingwa wa kihistoria wa mashindano hayo wakichukua kwa zaidi ya misimu mitano, walianza kwa kishindo mwishoni mwa wiki iliyopita katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa saa 10:30 jioni kwenye Uwanja wa Mirongo, Mwanza wakiwafunga mabingwa watetezi, Eagles vikapu 81-72.
Akizungumzia ushindi huo, Nahodha wa Profile, Basalile Mponjoli, alisema kikosi chao kimefanyiwa mabadiliko makubwa kwa kupandisha wachezaji wengi kutoka timu ya vijana ambao wana kasi, nguvu, vipaji na morali ya kushinda, jambo ambalo liliwasaidia kuhimili ushindani wa Eagles na kupata ushindi.
Alisema msimu huu wamedhamiria kurejesha ubingwa walioupoteza msimu uliopita, huku akitangaza kiama kwa wapinzani wao kwani wamejiandaa kushinda mechi zote na kutwaa ubingwa.
“Malengo yetu makubwa ni kuwa bingwa msimu huu tumeboresha timu kwa kupandisha vijana wengi kwa sababu baadhi ya wachezaji waandamizi wanabanwa na majukumu na kukosa mazoezi na mechi, kwa hiyo tunaamini hawa watatuongezea nguvu.”
“Ukijumlisha damu changa na mazoezi tunayofanya tunaamini itatulipa tuna timu yenye nguvu na kasi ambao wana matamanio na wako fiti, timu yoyote itakayokutana na Profile ijiandae kufungwa tunataka tushinde mechi zote mpaka tunachukua ubingwa,” alisema Mponjoli.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Mwanza (MRBA), Sunday Mtaki alisema licha ya ligi hiyo inayoshirikisha timu nane za wanaume kukabiliwa changamoto ya ukata lakini anaamini itakuwa na ushindani.
“Wikendi iliyopita tulianza ligi na itaendelea Jumapili (keshokutwa) tunajaribu kuweka ratiba vizuri lakini tutacheza kwa mtindo wa mzunguko na timu zote zitacheza playoff hadi hatua ya robo fainali, timu zifanye maandalizi ya kutosha tunategemea kupata ushindani wa kutosha,” alisema Mtaki.