Rais Samia Awakabidhi Wakulima wahanga ya Mvua ya Mawe Fidia ya Sh Mil 354 Kutoka NBC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amekabidhi hundi yenye thamani ya sh milioni 354 iliyotolewa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni fidia kwa wakulima wa zao tumbaku walioathirika na mvua za mawe katika msimu wa kilimo uliopita katika mikoa tofauti hapa nchini. Fidia hiyo inatokana na huduma ya bima ya kilimo inayotolewa na benki ya NBC kwa kushirikiana kampuni ya Shirika la Bima la Taifa (NIC)

Zaidi, Rais Samia amekabidhi pia bima ya afya kwa wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao cha mkoani Lindi kupitia huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima inayotolewa na benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Assemble Insurance.

Rais Samia amefanya makabidhiano hayo leo jijini Dodoma alipotembelea banda la NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi kuhusiana na huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo huduma za bima ya kilimo na bima ya afya mahususi kwa wakulima.

“Bima hii ya kilimo ni moja ya suluhisho muhimu katika kuwahakikishia wakulima kipato cha uhakika bila kuhofia changamoto nyingine zikiwemo zile za asili ikiwemo mvua za mawe.Nitoe wito kwa wakulima nchini kutumia vema fursa hii muhimu kwa kuhakikisha wanapata huduma hizi za bima ya kilimo na bima ya afya. Zaidi nawapongeza sana NBC na wadau wote wanaoshiriki kwenye mpango huu,’’ alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu huduma ya Bima ya Kilimo mbele ya Rais Samia, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema itasaidia kuondoa changamato ya hasara walizokuwa wakizipata wakulima kutokana na majanga mbalimbali yaliyo nje ya uwezo wao ikiwemo mafuriko, moto na mvua za mawe ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiathiri ustawi wa wakulima na kusababisha baadhi yao kuhofia kuwekeza kwenye sekta hiyo muhimu.

‘’ Hata hivyo Mheshimiwa Rais hatua hii ya NBC ni mwazo tu kwa kuwa huu ndio mwaka wa pili tangu waanze kutoa huduma hii na tayari mafanikio yanaonekana. Kama serikali tunaahidi kuendelea kuwaunga mkono katika utekelezaji mkubwa zaidi wa huduma hii lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba huduma hii ya bima ya kilimo inawafikia wakulima wengi zaidi.’’ alipongeza Bashe

Kwa mujibu wa Sabi wakulima walionufaika na malipo hayo wanatoka kwenye vyama vikuu vya ushirika 23 kutoka mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Mbeya, Katavi na Kigoma.

“Mbali na huduma huduma hizi za kibima, kama benki kupitia maonesho haya tumeendelea na utaratibu wetu wa kutoa elimu ya fedha na fursa mbalimbali za kibenki kwa wakulima sambamba na kutoa mikopo mbalimbali kwao ikiwemo mikopo ya zana za kilimo hususani mwa matrekta kwa wakilima mbalimbali waliokidhi vigezo na masharti ya mikopo hiyo,’’ aliongeza Sabi.

Akiwa bandani hapo Rais Samia pia alipata wasaa kufahamu huduma mbalimbali zitolewazo na benki hiyo mahususi kwa wakulima ikiwemo Akaunti ya Mifugo inayolenga kuwahudumia wadau wa sekta ya mifugo nchini huku pia akipata nafasi ya kuzungumza na wanufaika wa huduma hizo akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao Bw Hassan Mnumbe ambae chama chake kimekabidhiwa kadi ya bima ya afya kutoka benki hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (wa pili kulia) akimkabidhi Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege (Kushoto) mfano wa hundi yenye thamani sh milioni 354 iliyotolewa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni fidia kwa wakulima wa zao tumbaku walioathirika na mvua za mawe katika msimu wa kilimo uliopita katika mikoa tofauti hapa nchini. Fidia hiyo inatokana na huduma ya bima ya kilimo inayotolewa na benki ya NBC kwa kushirikiana kampuni ya Shirika la Bima la Taifa (NIC). Rais Samia amefanya makabidhiano hayo leo jijini Dodoma alipotembelea banda la NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (Kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi (wa tatu kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kaimu Mkeyenge.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi (Kulia) akifafanua kuhusu huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na benki hiyo mahususi kwa wakulima wakati Rais Samia alipotembelea banda la Maonesho la Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (Kushoto).

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw Theobald Sabi (kushoto) akikabidhi kadi ya Bima ya Afya kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao Bw Hassan Mnumbe (wa pili kushoto) akiwa ni mnufaika wa huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima inayotolewa na benki hiyo kwa kushirkiana na kampuni ya Bima ya Assemble Insurance. Makabidhiano hayo yamefanyika leo kwenye banda la maonesho la Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma.Wengine ni maofisa wa Kampuni ya Bima ya Assemble insurance Bi Lilian Deogratius (Kulia) na Bi Christina Luanda (wa pili kulia).

Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa (Alievaa kofia) akimpongeza mkulima Alberto Kacheza ambae ni mnufaika wa mkopo wa trekta kutoka benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Mahindra. Makabidhiano hayo yamefanyika leo kwenye banda la maonesho la Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma.Wengine ni pamoja na Mkuu wa Biashara ya Kilimo kutoka Kampuni ya Mahindra Bw Praveen Chandra pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo.

Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana (Katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa benki ya NBC wakiongozwa na Meneja wa Benki hiyo tawi la Dodoma Bi Happiness Kizigira (wa tatu kushoto) wakati Waziri huyo alipotembelea banda la maonesho la Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw Theobald Sabi (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kaimu Mkeyenge wakati Bw Mkeyenge alipotembelea banda la maonesho la benki hiyo lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma. Benki ya NBC inashirikiana na Shirika la Bima la Taifa (NIC) kutoa huduma ya Bima ya Kilimo kwa wakulima ambapo kwenye maonesho hayo wadau hao kupitia Rais Samia waliweza kukabidhi fidia yenye thamani ya sh milioni 354 kwa wakulima wa zao tumbaku walioathirika na mvua za mawe katika msimu wa kilimo uliopita katika mikoa tofauti hapa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw Theobald Sabi (kulia) akisalimiana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi Ruth Zaipuna wakati Bi Zaipuna alipotembelea banda la maonesho la benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma. Wengine ni pamoja Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kaimu Mkeyenge (Katikati) na Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa (Kushoto)

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw Theobald Sabi (kushoto) akisalimiana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB Bw Abdulmajid Nsekela wakati Bw Nsekela alipotembelea banda la maonesho la benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma.

Baadhi ya Maofisa wa Benki ya NBC wakitoa huduma mbalimbali za kibenki kwa wageni mbalimbali waliotembelea banda la maonesho la benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma.

Related Posts