RAIS wa Kenya, William Ruto leo Alhamisi amewaapisha mawaziri 19 aliowateua hivi karibuni huku zaidi ya nusu yao wakitajwa kuwa ni mawakili. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Kati ya mawaziri walioapishwa, wanane wana Shahada za Uzamili na Sheria. Mwanasheria Mkuu aliyeteuliwa Dorcas Oduor na Katibu wa Baraza la Mawaziri, Mercy Wanjau pia ni mawakili na kufanya jumla ya mawakili katika Baraza jipya la Mawaziri la Rais Ruto kufikia 10.
Chaguo lake linaonekana kama jibu kwa mapigo na vikwazo kadhaa vya kisheria ambavyo utawala wake umepata kwa karibu miaka miwili tangu aingie madarakani.
Baadhi ya maamuzi ambayo yametangazwa kuwa kinyume na yalitokana na sera zilizoidhinishwa katika ngazi ya Baraza la Mawaziri.
Kesi hizo zimekuwa nyingi na kuashiria uwezekano wa ushauri usio sawa wa kisheria kwa Rais na Mawaziri, ambao ni washauri wake wakuu wa masuala mbalimbali.
Mawakili katika Baraza la Mawaziri ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Prof Kithure Kindiki, Alice Wahome (Ardhi, Kazi za Umma, Nyumba na Maendeleo ya Miji), Opiyo Wandayi (Kawi na Petroli), Julius Ogamba (Elimu), Roselinda Tuya (Ulinzi), Rebecca Miano (Utalii), Kipchumba Murkomen (Masuala ya Michezo na Vijana) na Justin Muturi (Utumishi wa Umma).
Katika hotuba yake wakati wa hafla ya kuapisha mawaziri hao, Rais Ruto alisisitiza azma yake “kutumia kikamilifu fursa zote ndani ya miundo na mifumo yetu ya kisheria na kitaasisi kushauriana na kushirikiana na asasi za kitaifa za haki na sheria kwa nia ya kukuza ufanisi katika kuchunguza kwa haraka na kwa uthabiti kesi zote ndani ya muda maalum.”