MABOSI wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba ni kama jana Alhamisi ilibifu juu ya namba 28 ya kipa Aishi Manula baada ya kumtambulishia kipa mpya wa timu hiyo, Moussa Camara kabla ya pambano la Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kisha kubadilisha fasta na kumpa Mguinea huyo namba 26.
Katika orodha ya kikosi cha timu hiyo kabla ya pambano hilo la nusu fainali lililochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam na Simba kulala 1-0, Camara alitambulisha na jezi hiyo namba 28 ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitumiwa na Manula ambaye kwa sasa ana mgogoro na klabu hiyo.
Hata hivyo, wakati vikosi vikiingia uwanjani na kucheza pambano hilo, Camara alikuwa amevaa jezi namba 26 ambayo msimu uliopita ilikuwa ikitumiwa na beki wa kati, Kennedy Juma.
Mkanganyiko huo wa utambulisho wa jezi namba katika orodha ya awali ya kikosi hicho tofauti na ile aliyovaa kipa huyo mpya aliyesajiliwa wiki iliyopita akitokea AC Horoya ya Guinea, ilifanya baadhi ya mashabiki kutoa maoni tofauti, baadhi wakiamini Manula na Simba ndio basi tena ila mabosi wanazuga.
Manula aliyesajiliwa na Simba tangu mwaka 2017, safari hii hakuwa katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya ya timu hiyo iliyokuwa Misri, lakini hata kwenye utambulisho wa kikosi kipya cha msimu wa 2024-2025 alisahaulika kutambulishwa na baadaye Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally alitoa ufafanuzi, akisisistiza kipa huyo bado ni mali yao japo alisahaulika katika utambulisho wa kikosi hicho.
Mwanaspoti leo lilimtafuta Ahmed Ally ili atoe ufafanuzi wa kilichotokea Kwa Mkapa, lakini hakuweza kupokea simu ya Mwandishi wala kujibu meseji alizotumiwa.