Simba yafafanua ishu ya jezi ya Manula

HATIMAYE uongozi wa Simba kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, imetoa ufafanuzi juu ya jezi namba 28 inayotumiwa na kipa Aishi Manula ambayo alitambulishwa nayo kipa mpya Moussa Camara kwenye orodha ya kikosi hicho kabla ya mechi dhidi ya Yanga iliyopigwa jana Alhamisi.

Camara aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea AC Horoya ya Guinea, alitajwa kama atavaa jezi namba 28 katika orodha ya utambulisho wa kikosi kilichowekwa katika akaunti za mitandao ya kijamii za klabu hiyo, lakini alipoingia uwanjani alionekana akiwa na jezi namba 26 iliyokuwa ikitumiwa na Kennedy Juma aliyeondoka.

Jezi namba 28 kwa misimu saba sasa huwa inatumiwa na Manula ambaye ana mgogoro kwa sasa na klabu hiyo kiasi kwamba hakuwepo katika kambi ya maandalizi ya msimu wa 2024-2025 iliyokuwapo jijini Ismailia Misri na kwenye utambulisho wa kikosi cha msimu kwenye Tamasha la Simba Day alisahauliwa kabla ya uongozi wa Simba kufafanua kuwa walipitiwa tu, lakini kipa huyo namba wa Tanzania bado ni mali yao.

Kutokana na utata huo wa jana juu ya namba sahihi ya kipa Camara anayefahamika zaidi kama Spider, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amefafanua, kuna makosa yalijitokeza kwenye uandikwaji wa namba ya kipa huyo katika orodha ya wachezaji walioanza dhidi ya Yanga.

“Aliyeiandika lineup (orodha) ya kikosi kilichocheza jana alikosea, ila ukweli ni kwamba Camara atakuwa anatumia jezi namba 26, hilo lilirekebishwa jana hiyo hiyo, wakati wa mechi kwa kipa huyo kuvaa namba yake sahihi,” amesema Ahmed na kuongeza;

“Ufafanuzi huo unakwenda kuondoa sintofahamu iliyojitokeza awali, juu ya Camara atatumia jezi gani?. Kipa huyo atavaa jezi namba 26 iliyokuwa inavaliwa na beki aliyeondoka Kennedy Juma.”

Simba imemsajili kipa huyo raia wa Guinea, wiki iliyopi baada ya kuumia kwa Ayoub Lakred wakiwa kambini Misri na katika mchezo wa jana alionyesha kiwango cha hali ya juu dhidi ya mastaa wa Yanga, licha ya kuruhusu bao moja, kiasi cha kuwakuna mashabiki waliomshangilia mara baada ya pambano hilo la nusu fainali ya Ngao ya Jamii.

Katika mchezo huo Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 na kutinga fainali ambapo sasa itakutana na AzamFC iliyogawa dozi nono kwa Coastal Union ya mabao 5-2, huku Simba na Wagosi wenyewe watacheza mechi ya kusaka mshindi wa tatu, zote zikipigwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Related Posts