Wakati ukiendelea kutafakari matokeo ya Derby ya Kariakoo iliyopigwa jana kwa Simba kulala kwa bao 1-0 mbele ya watani zao Yanga, timu hizo mbili zitakutana tena Oktoba 19, mwaka huu kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Mchezo huo utakuwa wa duru ya nane ya ligi ambapo Simba itakuwa mwenyeji wa Yanga na katika ratiba ya awali iliyotolewa leo Agosti 9, 2024 na Bodi ya Ligi (TPLB) unatarajiwa kupigwa Uwanja mpya wa KMC Complex.
Ratiba hiyo imeonyesha Ligi Kuu itaanza rasmi Agosti 16, mwaka huu kwa mchezo mmoja kati ya Pamba Jiji na Tanzania Prisons mtanange utakaopigwa Dimba la CCM Kirumba Mwanza.
Mechi nyingine zitafuata, ambapo Agosti 17, Mashujaa itaikaribisha Dodoma Jiji, Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma na Namungo itakuwa mwenyeji wa Fountain Gate Uwanja wa Majaliwa Lindi.
Simba itatupa karata yake ya kwanza kwenye ligi msimu huu Agosti 18, itakapomenyana na Tabora United nyumbani kwenye Uwanja iliochagua kutumia wa KMC Complex na siku hiyo kule Sokoine Mbeya, Ken Gold itakuwa ikicheza na Singida Big Stars.
JKT Tanzania itaanza na Azam, Agosti 28 kwenye Dimba la Meja Isamuhyo, Dar es Salaam.
Mabingwa watetezi wa ligi, Yanga itaanza ligi Agosti 29 mwaka huu ikiwa ugenini katika Uwanja wa Kaitaba ikiikabili Kagera Sugar na kabla ya mchezo huo KMC itamenyana na Coastal Union Uwanja wa KMC.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo ya awali, ligi inatarajia kutamatika Mei 24, 2025 baada ya kila timu kukamilisha duru 30 za ligi.
Katika msimu ujao zitashuhudiwa timu mbili mpya zilizopanda kutokea Championship ambazo ni Pamba ya jijini Mwanza na KenGold ya Mbeya huku Mtibwa Sugar na Geita Gold zikikosekana baada ya kushuka daraja.
Ikumbukwe Bingwa wa msimu uliopita ni Yanga iliyobeba kwa misimu mitatu iliyopita mfululizo. Azam FC ilimaliza katika nafasi ya pili, Simba ikiishia namba tatu na Coastal Union kumaliza namba nne.
Timu shiriki msimu huu ni Yanga, Azam, Simba, Coastal, KMC, Tabora United, Namungo, Dodoma JIJi, Mashujaa, Kagera Sugar, Pamba, Ken Gold, Tanzania Prisons, JKT Tanzania, Fountain Gate na Singida Big Star.