Dar es Salaam. Wanawake watatu jasiri wametoa simulizi ya maisha yao katika sekta ya ujenzi, kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na wanaume.
Kina mama hao wakazi wa wilayani Ludewa mkaoni Njombe, wamechagua njia ya maisha inayohitaji nguvu na ujasiri wa hali ya juu.
Wamekuwa wakihama kutoka mkoa mmoja hadi mwingine nchini Tanzania, wakifanya kazi za kubeba zege, matofali, na vifusi kwenye maeneo ya ujenzi wa majengo.
Simulizi yao ni ushuhuda wa ujasiri na uthubutu wa wanawake ambao wanavunja mipaka ya kijinsia katika jamii.
Wanawake hao wabeba zege ni Furaha Fusi, Upendo Chaya na Secy Mwinuka wote wakazi wa Wilaya ya Ludewa mkaoni Njombe.
Mwananchi lilifanya mahojiano na wanawake hao wakiwa kazini eneo la Mwananyamala jijini Dar es Salaam wakijenga nyumba.
Furaha anasimulia kwamba, kukutana kwao kunatokana na kampuni ya Finehome ya Ludewa kuwakutanisha.Iliwapa ajira wakiwa tisa wakifanya kazi ujenzi kwa kutwa.
Hata hivyo, kutokana na changamoto nyingi, zikiwamo za hali ya hewa isiyotabirika na mazingira magumu ya kazi wengine waliachia wakabaki wao watatu.
Uchapakazi wao, Furaha anasema ni miongoni mwa sababu iliyowabakisha kazini, kwani kila mahali kampuni ilipopata kazi ilisafiri nao kwenda kuitekeleza.
Furaha anasema alianza kazi hiyo miaka mitano iliyopita baada ya kuachana na mume wake, ambaye alimtegemea kwa kila kitu kwa kuwa alimwachisha kazi yake ya awali ya ulinzi.
Anasema mume wake alimuondoa kazini baada ya kuoana akimweleza asingeweza kumvumilia kwenda lindo usiku.
“Nikiwa bado na mume wangu mwaka 2017 kampuni hii ilikuwa Ludewa ikijishughulisha na ujenzi. Nikaenda kuomba kazi ya kuchota maji nikawa nalipwa kwa kutwa,” anasimulia.
Anasema baada ya miaka miwili alipoachana na mume wake alikwenda kuomba kazi akapata ikiwa ni pamoja na kubeba zege na nyingine anazoendelea kufanya hadi sasa.
Furaha (34) anasema anaipenda kazi yake kwa kuwa inampa mahitaji yake muhimu, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wazazi na watoto wake watatu.
Anasimulia wawili kati ya hao wapo kwa baba yao na amekuwa akimtumia mzazi mwenzake fedha za matumizi licha ya kuwa anaishi na mwanamke mwingine.
“Tumezoea wanawake tunapoachana na wenzetu ndio tutumiwe hela, lakini mimi nafanya hivyo kwa mwanamume tuliyeachana kwa kuwa natambua yupo na watoto wangu lazima tusaidiane katika kuwalea,” anasema.
Upendo Chaya (20), yeye alianza shughuli za ujenzi mwaka 2019 baada ya kuacha kazi ya mama lishe, ambayo alikuwa akilipwa kati ya Sh2,000 na Sh3,000 kwa siku.
“Ni kazi ambayo ilikuwa hainilipi kutokana na majukumu niliyokuwa nayo ya kumlea mtoto pamoja na bibi yangu ambaye ndiye naishi naye kama mama kwa kuwa alinilea tangu nikiwa mtoto,” anasimulia.
“Niliposikia kuna kampuni ya ujenzi inahitaji wafanyakazi niliomba kazi, ninashukuru hadi sasa nazunguka mikoa mbalimbali kufanya kazi za ujenzi,” anasema.
Upendo anasema harakati za kazi hiyo zinamwezesha kupata kipato licha ya kwamba kuna wakati huwa mbali na familia hata kwa miezi mitatu kulingana na ukubwa na uzito wa kazi.
Anasema kazi inapoanza hulipwa hadi Sh15,000 kwa siku, na kwa kadri kazi zinavyoelekea ukingoni hawakosi Sh10,000 kwa siku.
Secy Mwinuka, anasimulia alianza kazi za ujenzi wakati mtoto akiwa na mwaka mmoja na sasa ana miaka minne.
Tofauti na wenzake, Secy anasema alitafutiwa kazi na mume wake ambaye alianza kufanya kazi katika kampuni hiyo kwa muda.
Anasema hadi sasa wanafanya kazi pamoja katika kampuni hiyo.
Ili kupunguza gharama za maisha, anasema kila wanapokwenda kujenga na wanapotambua ujenzi utachukua muda mrefu hupanga chumba.
Anasema mara nyingi hulipa kodi ya miezi mitatu na kuishi kama familia nyumbani.
Anasema wakati mtoto wake alipokuwa akinyonya, alikuwa akipelekewa kazini kwa ajili ya kumnyonyesha. Alifanya hivyo hadi alipotimiza miaka miwili.
Utani kwa wanawake hawa wanasema ni moja ya changamoto wanazokabiliana nazo kazini.
Secy anasema iwapo hukuzoea utani unaweza kupigana na mtu.
Suala la malipo ni changamoto nyingine, akieleza pale bosi wao anapocheleweshewa malipo kutoka kwa mteja nao husota kwa kutolipwa kwa wakati.
“Hata hivyo, huwa tunavumilia kwa kuwa bosi wetu tunamuelewa hajawahi kutudhulumu, lakini ndio hivyo nyumbani ukishindwa kutuma hela na wanajua upo kazini hawakuelewi hasa sisi tulioacha watoto,” anasema Secy.
Kwa upande wake, Furaha anasema kuna changamoto ya kuombwa kuanzisha uhusiano wa mapenzi.
Hata hivyo, anasema ni jukumu la mhusika kutambua amekwenda kufanya nini, vinginevyo mtu unaweza kujikuta umejiingiza kwenye uhusiano na kila mtu.
Sylvest Noel, bosi wa wanawake hao amesema amekuwa akizunguka nao kila mahali anapopata kazi.
Anasema licha ya kulipwa kiwango kidogo cha posho, wamekuwa wakijituma na baadhi wamenunua viwanja kwa kazi hiyo.
“Hii kazi kwa wanawake inalipa kama utajua umekuja kufanya nini, na hawa nawapongeza wanajituma kwelikweli, kwani kuna wengine huwa wakija kwa shughuli zingine na ninapowashtukia huwa nikiachana nao mara moja,” amesema Noel.
Daniel Yohana, anayefanya kazi na wanawake hao anasema wamekuwa wakiishi nao kwa upendo katika kipindi chote cha kazi.
Tofauti na wanaume, amesema wanawake ni wanyenyekevu hata pale wanapopishana kauli huwaita na kuzungumza badala ya kupigana.
Simulizi ya Furaha, Upendo na Secy ni ushuhuda wa ujasiri na uthubutu wa wanawake ambao wanavunja mipaka ya kijinsia katika jamii.
Kutokana na kujiamini, bila kujali vikwazo wanavyopitia wamesema wanahakikisha wanajitafutia kipato kwa ajili ya kusaidia familia zao.