TRA ilivyojipanga kutanua wigo wa mapato

Dar es Salaam. Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amesema mkakati unaondelewa na kuoanisha mifumo ya mamlaka hiyo na taasisi nyingine za Serikali utasadia kupanua wigo wa kodi nchini.

Kupitia mpango huo wa kufanya mifumo isomane, amesema wataweza kubaini mwenendo na ukubwa wa biashara za wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali na hatimaye watawasajili na kuwatatoza kodi kwa kiwango anachostahili.

Mkakati huo huenda utajibu sehemu ya malalamiko ya wafanyabiashara nchini, wanaolalamikia wigo mdogo wa kodi nchini, jambo linalosababisha wingi na ukubwa wa kodi kwa wafanyabiashara wachache.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), kwa sasa nchini kuna jumla ya walipakodi chini ya milioni tatu.

Mwenda ameeleza mikakakti hiyo leo, Ijumaa Agosti 9, 2024 wakati wa uzinduzi wa programu tumizi ya Sikika itakayotumiwa na wananchi kutoa maoni, mapendekezo na malalamiko na kumfikia moja kwa moja Kamishna Mkuu.

Kwa mujibu wa Mwenda, mifumo ikishasomana zitajulikana taarifa za nani anafanya nini na atakapogundulika.

Ametoa mfano kuwa mifumo ya mizani inayoendeshwa na Tanroads ikishasomana na ya TRA, inaweza kuwasaidia kujua ukubwa wa mizigo inayopita na hivyo kufuatilia kiwango cha kodi kinachopaswa kulipwa.

“Mifumo hii itafanya kumjua mfanyabiashara kwa mfano, wale wanaosafirisha mizigo kwenye mizani tutaona amepita mara ngapi na anapitisha mzigo gani kwa ukubwa gani na akiwa anastahili tutamsajili,” amesema.

Amekiri uwepo wa wigo mdogo wa kodi kwa upande wa wafanyabiashara, ingawa kila Mtanzania katika kila bidhaa anayonunua analipa kodi.

“Mifumo hiyo pia itawezesha kuirasimisha sekta isiyo rasmi ambayo ni kubwa na namna gani tunaitambua na kuiweka katika wigo wa kuchangia ni jambo tunaloshughulikia,” amesema.

Mwenda amesema mpango huo unaoendelea unalenga kuoanisha mifumo 300 ya taasisi mbalimbali za Serikali, 80 ikiwa tayari imesomana, shughuli ambayo itakamilika Januari mosi mwakani.

Sambamba na hilo, amesema idadi ya sasa ya watumishi TRA ni kubwa baada ya kuongezwa, hivyo itasaidia kuwafikia wafanyabiashara wengi na kuwabaini wanaostahili kusajiliwa na kuwa sehemu ya walipakodi.

Akizungumzia hilo alipozungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Livembe amesema kiu yao kuona hilo linatekelezwa.

Ametoa angalizo utekelezwaji wa hilo uzingatie kuongeza vyanzo vipya vya kodi vitakavyotokana na watu wapya, badala ya vyanzo vipya kwa watu walewale.

“Kuna wakati TRA wanasema wamepanua wigo wa kodi kwa kuongeza kodi au kutunga kodi mpya kwa walipakodi walewale, hii mifumo isiguse hilo, wakatafute walipakodi wapya ndiyo kiu yetu,” amesema.

Amesema inashangaza Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 60 ina walipakodi milioni mbili na kati yao wanaolipa kwa hiari ni 500,000 wakati Kenya yenye watu milioni 32 walipakodi ni milioni tisa.

Mwenda amesema wanashirikiana na mamlaka za serikali za mitaa kuwafikia wafanyabiashara waliopo katika ngazi hizo, ambao kwa sehemu kubwa si walipakodi.

Kitu kingine wanachokifanya kuongeza wigo wa kodi, amesema ni kujenga hamasa ya wafanyabiashara wajisikie kuwa sehemu ya sekta rasmi kwa kuongeza vivutio.

“Tunataka kuondoa faida zinazofanya wang’ang’ane kutokuwa rasmi ili waone umuhimu wa kuwa rasmi,” ameeleza.

Mbali ya hayo, amesema anaendelea kukutana na makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na mabalozi, kuhakikisha anasikiliza na kutatua changamoto zao ili kuongeza ulipaji kodi wa hiari.

Jambo jingine, amesema atasimamia kukomesha vitendo vya ukwepaji kodi na kuhakikisha kila anayestahili analipa kwa kiwango sahihi bila kumwonea wala kumpendelea.

Mwenda pia amesema wanafikiria kulifanya soko la Kariakoo kuwa kanda maalumu ya kikodi, hatua itakayotanguliwa na kuboresha mazingira ya biashara sokoni hapo.

Katika kushughulikia changamoto za wafanyabiashara sokoni hapo, amesema umeandaliwa utaratibu wa kukutana nao mara tatu kila mwezi.

Kuhusu programu ya Sikika, amesema itamwezesha mfanyabiashara au mwananchi kutoa maoni, malalamiko na ushauri wa kikodi kwa TRA na moja kwa moja utamfikia kamishna ili kuongeza ubora wa huduma.

Amesisitiza katika utoaji wa taarifa hizo kutakuwa na usiri mkubwa wa mtoa taarifa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amebainisha changamoto za sekta ya habari katika mifumo ya kodi, masuala ambayo Mwenda amesema wameyachukua na watayafanyia kazi.

Related Posts