BAADA ya wikendi iliyopita nchi kuwa bize kwa matamasha ya Simba, Yanga jijini Dar es Salaam na Azam Kigali, Rwanda, kesho ni zamu ya Jiji la Mwanza na litapokea wageni mbalimbali kwa ajili ya tamasha la klabu ya Pamba Jiji itakayokuwa inahitimisha kilele cha tamasha la Pamba Day.
Tamasha hilo litafanyika kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa kwa klabu hiyo kutambulisha kikosi na benchi la ufundi la msimu ujao, likisindikizwa na burudani za muziki kutoka kwa Harmonize, Fid Q, Kala Jeremiah na wengine, kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Vital ‘O ya Burundi.
Hamasa za tamasha hilo zilizozinduliwa Agosti 4, mwaka huu zikihusisha kuuza tiketi na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufungua matawi, kutoa msaada kwa wenye uhitaji na kuchangia damu, tayari zaidi ya tiketi 20,000 zimeshauzwa huku uwanja huo ukiwa na uwezo wa kuingiza mashabiki zaidi ya 30,000.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi Pamba Day, Amina Makilagi alisema mpaka mwishoni mwa wiki iliyopita walikuwa wameuza tiketi 20,000 na matumaini yao ni hadi kesho tiketi zote 30,000 zitakuwa zimekwisha na kupata mapokezi makubwa ya watu watakaohudhuria tamasha hilo.
Alisema tamasha hilo ni la kihistoria kwa klabu ya Pamba ambayo imerejea Ligi Kuu baada ya miaka 23, hivyo wakazi wote wa Mwanza na mikoa jirani wanapaswa kujumuika kuiunga mkono timu yao na kupata burudani.
“Tumefanya hamasa mbalimbali kwa ajili ya tamasha letu na tunaamini litakuwa na mwitikio mkubwa, tunatarajia mageti ya uwanja yatafunguliwa kuanzia saa 12 asubuhi ili watu waingie mapema, pia tumejiandaa kwa ulinzi na usalama kwa mashabiki watakaohudhuria,” alisema Makilagi.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Martin Sawema maandalizi ya tamasha hilo yanakwendaje vizuri na litajumuisha burudani mbalimbali zikiwemo za wasanii wa Mwanza, michezo ya maveterani, waandishi wa habari wa Mwanza na Dar es Salaam na kuhitimishwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Vital ‘O ya Burundi.