Ukraine inaendeleza mashambulizi yake dhidi ya Urusi – DW – 09.08.2024

Mashambulizi ya Ukraine yaliyoanza siku ya Jumanne, katika eneo hilo la mpakani la Kursk lililoko Magharibi mwa taifa hilo, yanasemekana kuwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika katika ardhi ya Urusi tangu Moscow ilipoivamia mwezi Februari mwaka 2002.

Urusi inasema zaidi ya wanajeshi 1000 pamoja na darzeni mbili ya magari na vifaru vya kivita vya Ukraine, vilihusika katika shambulizi hilo. Wizara ya mambo ya dharura ya Urusi imetangaza hali ya hatari katika eneo hilo la Kursk.

Urusi bado yapambana na wanajeshi wa Ukraine waliovuka mpaka

Kiev haijakiri rasmi kutekeleza operesheni hiyo lakini rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, alisema katika hotuba yake jana Alhamisi kwamba Urusi ni lazima ihisi matokeo ya Uvamizi wake.

Kwengineko Ukraine imesema imetekeleza shambulizi kubwa zaidi katika kambi ya kijeshi ya Urusi katika eneo la Lipetsk ikiwa ni kilomita 280 kutoka mpaka wa Urusi na Ukraine. Gavana wa eneo hilo Igor Artamonov, amekiri kuwepo kwa mashambulizi hayo usiku kucha huku vyombo vya habari navyo vikiripoti kuteketea kwa uwanja wa ndege wa kambi hiyo.

Raia waondoka karibu na kambi iliyoshambuliwa

Kursk  | Ukraine
Watu wanaoishi karibu na kambi ya kijeshi iliyoshambuliwa mjini Kursk wameamriwa kuondoka kuelekea eneo salamaPicha: IMAGO/SNA

Kufuatia tukio hilo Artamonov, alifuta shughuli zake zote katika eneo hilo na kutoa mara moja amri kwa wakaazi wanaoishi karibu na kambi hiyo ya kijeshi kuondoka. Huku hayo yakiarifiwa wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imeziharibu droni 75 za Ukraine, zikiwemo 19 katika eneo la Lipetsk na Saba katika eneo la Kursk ambalo ni kitovu cha uvamizi wa ukraine dhidi ya Urusi. Pia droni kadhaa zilizoelekezwa katika eneo linalokaliwa na Urusi la Crimea ziliharibiwa. 

Urusi imesema inaendelea kutumia roketi na mashambulizi ya angani kujaribu kuwasogeza nyuma wanajeshi wa Ukraine. Kulingana na rais wa taifa hilo Vladimir Putin, Uvamizi unaoendelea kwa siku ya tatu ni uchokozi mkubwa unaofanywa na Kiev dhidi ya taifa lake, huku yeye na pamoja na Jenerali mkuu wa kijeshi wakiapa kuisambaratisha operesheni ya kiev.

Vikosi vya Ukraine vyajipenyeza ndani ya Urusi

Wizara ya afya imesema raia 66 wakiwemo watoto 9 wameuwawa katika operesheni hiyo ya Ukraine dhidi ya Urusi. Marekani na Umoja wa Ulaya zimeendelea kusisitiza kwamba Ukraine ina haki ya kujilinda kutokana na uchokozi wa Urusi bila ya moja kwa moja kuzungumzia kinachoendelea kwa sasa.

Mapigano mengine makali yameripotiwa karibu na mji wa Sudzha, ambako kuna mitambo ya kusafirisha gesi ya Urusi kuelekea Ukraine, jambo ambalo limezusha wasiwasi wa kusimamishwa kwa upelekaji nishati hiyo barani Ulaya.

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Chanzo: afp, ap, reuters

Related Posts