Umoja wa Ulaya waunga mkono juhudi za kusitisha vita Gaza – DW – 09.08.2024

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen ameandika Ijumaa katika ukurasa wake wa X kuwa vita vya Gaza vinapaswa kusitishwa sasa, kauli inayoongeza shinikizo la kimataifa la kutaka kusitishwa vita kati ya Israel na Hamas.

Amesema hiyo ndiyo njia pekee ya kuokoa maisha, kurejesha matumaini ya amani na kuhakikisha usalama wa kurejeshwa watu wanaoshikiliwa mateka.

Von der Leyen amesema anaunga mkono juhudi zinazoongozwa na Marekani, Misri na Qatar za kusaidia kupatikana kwa amani na utulivu katika eneo hilo.

Israel yakubali kurejea kwenye mazungumzo

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilisema Alhamisi kuwa nchi hiyo imekubali kurejea kwenye meza ya mazungumzo ikiwa ni katika kutafuta usitishwaji wa mapigano Gaza yaliyopangwa kufanyika Agosti 15, kwa maombi ya wapatanishi wa Marekani, Qatar na Misri, huku mvutano wa kikanda ukiongezeka na kuwepo wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuzuka vita kamili.

Aidha, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amezitolea wito Israel na Hamas kuanza tena mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza, na makubaliano ya mpango wa kubadilishana wafungwa na wanaoshikiliwa mateka.

Wito kama huo umetolewa pia na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ambaye amesema nchi yake inaunga mkono kikamilifu juhudi za upatanishi katika vita baina ya Israel na Hamas.

Wapalestina wakiondoka Khan Yunis
Wapalestina wakiondoka Khan YunisPicha: Rizek Abdeljawad/Xinhua/IMAGO

Miito inatolewa wakati ambapo jeshi la Israel likitoa amri mpya ya watu kuondoka kwenye baadhi ya maeneo ya mji wa kusini wa Khan Yunis. Jeshi la Israel limeanzisha Ijumaa operesheni mpya za kijeshi huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Huku hayo yakijiri, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu katika Umoja wa Mataifa, Volker Türk amekosoa vikali matamshi ya Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, ambaye alisema kuwa ni haki kusababisha njaa kwa Wapalestina.

Kauli ya waziri wa fedha Israel yakosolewa

Msemaji wa ofisi inayosimamia haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Jeremy Laurence amesema kamishna Türk ameshangazwa na kauli hiyo.

“Tamko hili la moja kwa moja na la hadharani linahatarisha kuchochea uhalifu mwingine wa kikatili. Kauli kama hizo, hasa za viongozi wa umma, zinapaswa kukomeshwa mara moja, zichunguzwe na ikibainika kuwa ni uhalifu, lazima ashtakiwe na kuadhibiwa,” alisisitiza Laurence.

Laurence amesema kauli ya kuwaacha Wapalestina milioni mbili huko Gaza wafe kwa njaa hadi watakaporejeshwa nyumbani mateka ambao bado wanashikiliwa na kundi la Hamas, inaweza kuchochea chuki dhidi ya raia wasio na hatia.

Jengo likiwa limeharibiwa kwa shambulizi la anga la Israel huko Naqoura, Lebanon
Jengo likiwa limeharibiwa kwa shambulizi la anga la Israel huko Naqoura, LebanonPicha: Ali Hashisho/Xinhua/picture alliance

Katika eneo la mapambano, jeshi la Israel limesema Ijumaa kuwa limewaua wapiganaji wawili wa Hezbollah, kusini mwa Lebanon, huku kundi hilo likithibitisha vifo vya wapiganaji wake watatu hadi sasa.

Jeshi hilo limesema limeishambulia kambi ya kijeshi ya wanamgambo wa Kishia, huko Naqoura, eneo ambalo haliko mbali sana na mpaka wa Israel.

Hata hivyo, kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, wakati linathibitisha vifo hivyo, halikusema sehemu au wakati ambapo vifo hivyo vimetokea. Kundi hilo badala yake limedai kuwa limefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi kaskazini mwa Israel.

(AFP, DPA, Reuters)

Related Posts