Dar es Salaam. Wakati matarajio ya Watanzania juu ya bima ya afya kwa wote kuanza Julai mosi mwaka huu ‘kuota mbawa’ baada ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2024/2025 yaliyowasilishwa bungeni kutoonyesha mwelekeo wa kuanza hivi karibuni Britam Insurance Tanzania na Benki ya Afrika wamekuja na suluhu.
Britam na BOA zimeingia ushirikiano ili kuongeza upatikanaji wa huduma za bima za afya Tanzania ziitwazo ‘Amani Health’ na ‘Afya Care’.
Ushirikiano huo unalenga kuongeza wigo mpana kwa wateja wa ‘Bank of Africa’ ili kuhakikisha kuwa watu binafsi, familia, wafanyabiashara na vikundi rasmi wanapata huduma za afya zenye unafuu na viwango.
Mkurugenzi Mtendaji wa Britam, Farai Dogo amesema kuwa, “Tunafuraha kuungana na Bank of Africa nchini Tanzania ambapo tumeweza kuwaletea wateja wao huduma hizi muhimu za ‘Afya Care’ na ‘Amani Health’. Ushirikiano huu unaendana na dhamira yetu ya kuhakikisha tunatoa huduma bora za afya kwa watanzania wote. Hivyo ushirikiano huu utatuwezesha kuwafikia watu wengi zaidi na kuwapa ulinzi wanaohitaji ili waishi maisha bora zaidi.”
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa Tanzania, Esther Cecil Maruma, amesema “Ushirikiano wetu na Britam Insurance Tanzania ni uthibitisho wa ari yetu ya kutoa huduma za kipekee kwa wateja wetu, kupitia ‘Afya Care’ na ‘Amani Health’. Hii sio tu kwamba tunaboresha utoaji wa bidhaa zetu lakini pia tunahakikisha kwamba wateja wetu wanapata huduma muhimu za afya. Mkakati huu unaonesha dhamira yetu ya kuboresha ustawi kwa wateja wetu na jamii inayotuzunguka.”
Naye, George Mwita, Meneja wa Idara ya Afya, Britam Insurance Tanzania, amesema “Tunaamini kwamba ushirikiano huu utaongeza kiwango kipya cha bima ya afya nchini Tanzania.”
Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ulipitishwa na Bunge la Novemba mwaka jana kabla ya kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa sheria kamili Desemba Mosi 2023 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
Kabla ya kupitishwa na Bunge, muswada huo ulikwama mara kadhaa baada ya wabunge na Spika wa Bunge hilo, Dk Tulia Ackson kuonyesha shaka kwenye baadhi ya vifungu vya muswada huo, hasa vyanzo vya fedha kwa wasio na uwezo wa kuchangia.
Muswada uliporudi bungeni kwa mara nyingine, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitaja vyanzo mbalimbali vya mapato vitakavyogharamia watu hao wasiojiweza.
Vyanzo alivyovitaja na Bunge likaupitisha ni mapato yatokanayo na vipodozi, vinywaji vikali, michezo ya kubahatisha, vinywaji vyenye kaboni, mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki, fedha zitokanazo na Bunge, mapato yatokanayo na uwekezaji wa mfuko, zawadi na misaada kutoka kwa wadau.