Mirerani. Walemavu wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamelalamikia kitendo cha mlemavu mwenzao Fatuma Saidi (28) kuuawa kwa kuchinjwa shingoni na mwanaume aliyekuwa anaishi naye.
Mwenyekiti wa walemavu wilayani Simanjiro, Robert Matheus akizungumza na Mwananchi digital amesema anasikitishwa kwa tukio hilo la mauaji lililotokea leo Ijumaa saa moja asubuhi, Agosti 9, 2024 kitongoji cha Kilimanjaro.
Matheus amesema wamesikitishwa na kitendo cha mlemavu mwenzao Fatuma kudaiwa kuuawa kwa kuchinjwa shingoni na mwanaume aliyekuwa anaishi naye anayefahamika kama Amosi John (29).
“Huyu dada alikuwa mlemavu wa mguu na mkono na alikuwa mpambanaji ila huyu mwanaume amekatisha ndoto yake aliyokuwa nayo kwa kumfanyia ukatili mkubwa wa kumuondoa duniani kwa kumchinja,” amesema.
Jirani wa Fatuma aitwaje Sharon Samwel amesema kila mara watu hao waliokuwa wanaishi kwenye nyumba moja, walikuwa wanagombana mara kwa mara.
Sharon amesema Fatuma alishawahi kumfikisha Amos polisi na akapelekwa magereza siku 21 ila mwishowe akamsamehe wakaendelea na maisha yao.
Ndugu wa marehemu huyo, Elihuruma Eliafia amesema Fatuma ni mama yake mdogo na amesikitishwa na mauaji hayo ya kuchinjwa kwani alikuwa anajituma na huyo mwanaume wake alikuwa tegemezi kwake.
“Licha ya ulemavu wake alikuwa mpambanaji anajituma na huyo mwanaume aliyekuwa anaishi naye alikuwa analishwa na kulipiwa kodi ila mwishowe amemuua,” amesema.
Mama mwenye nyumba wa Fatuma aitwaye Upendo Swai, amesema tangu jana kwenye Sikukuu ya Nane nane walikuwa wanataniana na Fatuma ila leo asubuhi akasikia kelele na kufika kwenye chumba chao.
“Nikamuuliza huyu mwanaume aliyekuwa anaishi naye hii damu ya nini mbona Fatuma haonekani akadai kuwa Fatuma anaumwa na damu zinamtoka puani,” amesema.
Amesema baada ya tukio hilo Amos alitaka kukimbia ila majirani walimkamata na tukatoa taarifa kwa mkuu wa kituo cha polisi Mirerani Eusobio Nyalifa ambaye alifika mara moja na askari wake wakamkamata.
Mwenyekiti wa walemavu wa mji mdogo wa Mirerani, Martin Aloyce ameiomba Serikali ichukue hatua kali kwa sababu Amos ameshakamatwa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi mwandamizi SACP George Katabazi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Agosti 9 mwaka 2024 na wanamshikilia mtuhumiwa huyo.
Kamanda Katabazi amesema wanamshikilia Amos John (29) kwa tuhuma za mauaji ya Fatuma kwa kutumia kitu chenye ncha kali na wanaendelea na mahojiano naye juu ya tukio hilo.
“Chanzo halisi cha mauaji haya bado hakijajulikana mara moja, ila uchunguzi wa awali unonyesha kuwa Amosi alikuwa amekunywa pombe na kusababisha kutenda mauaji hayo,” amesema kamanda Katabazi.