Morogoro. Hamis Nguku, mwanafunzi mwenye ulemavu wa viungo ambaye amekuwa anatumia miguu kuandika, kula, na kufanya shughuli zake nyingine, ameishukuru kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) kwa kurusha habari zake, ambazo zilipelekea kupata mfadhili aliyemnunulia mahitaji muhimu ya shule.
Nguku, ambaye ni mkazi wa Mlimba katika Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, alipata ufadhili kutoka kwa taasisi ya Kalamu Education Foundation (KEF) ya jijini Dar es Salaam.
Habari zake zilirushwa kwenye gazeti la Mwananchi na mitandao ya kijamii, jambo ambalo liligusa taasisi hiyo kwa maisha aliyokuwa akiishi.
Nguku, pamoja na kuwa na maendeleo mazuri darasani, pia ana kipaji cha kuchora.
Katika habari hiyo kijana huyo ambaye katika matokeo ya kidato cha nne alipata ufaulu wa daraja la pili, kwa sasa anasoma katika Shule ya Sekondari ya kilimo Kilosa, alieleza namna familia yake ilivyokosa uwezo wa kumtafutia mahitaji ya shule ikiwemo sare za shule, michango pamoja na vifaa mbalimbali.
Kijana huyo katika habari hiyo pia alieleza kuwa mama yake mzazi alifariki dunia yeye akiwa na umri mdogo na mpaka sasa amefika kidato cha tano amekuwa akilelewa na bibi yake ambaye naye ni mzee, baada ya baba yake kumtelekeza kwa kile alichodai ni kutokana na hali yake ya ulemavu.
Baada ya habari hiyo kusambaa taasisi ya KEF on ilianza jitihada za kumtafuta kijana huyo kupitia kwa uongozi wa shule anayosoma, kisha ikaorodhesha mahitaji yote ya kumwezesha kijana huyo kuendelea na shule.
Wakati taasisi hiyo ikijipanga kumsaidia, Serikali ya Wilaya ya Mlimba ilimpeleka kijana huyo kwenye shule hiyo, ambapo aliendelea kusoma hadi mapema wiki hii KEF ilipomfikishia kijana huyo mahitaji hayo.
Akizungumza na Mwananchi, Nguku amesema pamoja na kuishukuru Mwananchi, pia ameishukuru taasisi hiyo kwa kuguswa na habari zake na kuamua kumsaidia.
“Naishukuru kampuni ya Mwananchi Kwa kunitangaza lakini kipekee kabisa naishukuru hii taasisi ya Kalamu Education Foundation kwa kuguswa na habari zangu na kuamua kunisaidia ambapo kwa sasa nasoma bila ya kikwazo chochote,” amesema.
Nguku ambaye anasoma mchepuo wa sanaa, ameweka ahadi kwa uongozi wa taasisi hiyo kuwa atafanya vizuri katika masomo yake na kufaulu mtihani wa kidato cha sita huku akiendelea kusimamia ndoto yake ya kuwa mchoraji maarufu nchini.
Mwakilishi wa KEF, Mohamed Kamlagwa amesema pamoja na msaada huo, taasisi hiyo itaendelea kuwa karibu na kijana huyo ili kuhakikisha anamaliza kidato cha sita bila vikwazo vyovyote.
“Binadamu wote ni sawa na tunathamini kila mmoja, tofauti ya maumbile haimfanyi mtu mwenye tofauti na ashindwe kupata haki zake ikiwa ni pamoja na elimu, hivyo tutaendelea kumsaidia na tutahakikisha hata vitabu anapata kwa ajili ya kujisomea na hata kama kutakuwa na gharama ya masomo ya ziada wakati wa likizo, tutamsaidia kadri mwenyezimungu atakavyotuwezesha,” amesema Kamlagwa
Mkuu wa shule hiyo, Mariam Msemakweli amesema Nguku ni mwanafunzi msikivu na mtulivu akiwa darasani na hata nje ya darasa na pia yuko vizuri katika masomo yake.
“Mbali ya kuwa mwanafunzi anayefanya vizuri darasani pia ana kipaji cha kuchora picha mbalimbali zikiwemo za viongozi na kwa maendeleo yake darasani naamini atafanya vizuri katika mtihani wake wa kidato cha sita,” amesema Msemakweli.
Akielezea hali ya ulemavu wake, Msemakweli amesema Hamisi hawezi kufanya shughuli yoyote kwa kutumia mikono bali shughuli zake zote anafanya kwa kutumia miguu.
Amesema kutokana na ukarimu na ucheshi wake mara nyingi amekuwa akipata msaada kutoka kwa wanafunzi wenzake kama kufua na kubeba ndoo ya maji.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.