Arajiga apewa fainali Ngao ya Jamii, Kayoko Simba vs Coastal

MWAMUZI Ahmed Arajiga kutoka Manyara, ameteuliwa kuchezesha fainali ya Ngao ya jamii kati ya Yanga dhidi ya Azam utakaopigwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.

Yanga imepata tiketi hiyo baada ya kuwaondoa Simba kwa kuichapa bao 1-0, huku Azam wakishinda 5-2 dhidi ya Coastal Union.

Arajiga ambaye alichezesha nusu fainali ya kwanza ya Ngao ya Jamii kati ya Azam dhidi ya Coastal, atasaidiwa na Frank Komba kutoka Dar es Salaam na Mohammed Mkono wa Tanga.

Mkono anarudi tena kwenye mchezo huu baada ya kuwepo katika nusu fainali ya pili ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga iliichapa Simba akiwa mwamuzi msaidizi namba moja.

Amina Kyando wa Morogoro atakuwa mwamuzi wa akiba kwenye mchezo huo huku Soud Abdi (Arusha) akipewa jukumu la kuwatathimini waamuzi hao. Hawa nao walikuwepo katika mchezo wa Yanga dhidi ya Simba kwenye majukumu yao hayohayo.

Naye mwamuzi Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam amepewa jukumu la kuamua mchezo kati ya Simba na Coastal Union wa kusaka nafasi ya tatu katika Ngao ya Jamii.

Mchezo huo utakaoanza saa 9:00 alasiri kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Kayoko ataisaidiwa na Glory Tesha atakayekuwa mwamuzi msaidizi namba moja, Hamdan Said ni mwamuzi msaidizi namba mbili, wakati Isihaka Mwalile (Dar es Salaam) akiwa mwamuzi wa akiba huku Issaro Chacha (Mwanza) atakuwa mtathimini wa waamuzi.

Related Posts