ATIWA MBARONI KWA MAUAJI YA MTOTO WA MIAKA 7 NA KUFICHA MWILI WAKE KWENYE SHAMBA LA MIGOMBA.

NA WILLIUM PAUL, ROMBO.

JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mtu mmoja mwanaume Mkazi wa Kijiji cha Mahango wilayani Rombo kwa tuhuma za kumfanyia matendo ya ukatili, udhalilishaji na kumuua kwa kumnyonga mtoto wa kiume aitwaye Amedeus Laurent, (7), na kuficha mwili wake kwenye shamba la migomba.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, SACP Simon Maigwa alisema kuwa, Mama mzazi wa mtoto huyo alifika katika kituo cha Polisi Agosti 6 mwaka huu na kutoa taarifa kuwa
mtoto wake haonekani tangu Agosti 5 majira ya saa kumi na mbili jioni mtoto.

Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi na siku hiyo hiyo lilipata taarifa kuwa mtuhumiwa huyo alionekana akiwa na mtoto huyo.

Kutokana na taarifa hiyo mtuhumiwa huyo alikamatwa lakini alipoulizwa alikana hakuwahi kuwa karibu na mtoto huyo na aliendelea kuhojiwa ambapo Agosti 9 mwaka huu Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuupata mwili wa mtoto huyo.

Baada ya mtuhumiwa kufahamu kuwa mwili wa mtoto umepatikana amekiri kufanya uhalifu huo.

Jeshi la Polisi linaendelea kukamilisha taratibu zingine za kiuchunguzi ili mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani.

Aidha Jeshi hilo limetoa onyo kali kwa Wananchi wanaoendelea kujihusisha
na matendo ya udhalilishaji, ukatili na mauaji na halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu yeyote atakajihusisha na matendo ya kikatili na uhalifu mwingine.

Pia wameitaka jamii kutoa ushirikiano kuwafichua wahalifu kama hawa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Related Posts