Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema wanatamani kuona vijana wengi wakiingia bungeni na Baraza la Wawakilishi na hivyo watawaunga mkono vijana wote watakaogombea nafasi hizo.
Dk Mwinyi, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar amesema Serikali itaongeza ajira nyingi za vijana kadri inavyowezekana ili kuondoa changamoto ya ajira na kuongeza fungu la mikopo ili vijana waweze kujiajiri.
Ametoa kauli hiyo leo, Agosti 10, 2024, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Kijana na Kijani” ya Umoja wa Vijana (UVCCM) yenye kaulimbiu isemayo “Tunazima zote na kuwasha ya kijani” katika Uwanja wa Amaan Complex Zanzibar.
Dk Mwinyi amesema kutokana na hamasa hiyo iliyofanywa na vijana, hana wasiwasi tena kwamba mwaka 2025 watawapiga wapinzani wao kipigo ambacho hawajawahi kuona, akimaanisha ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge, na madiwani.
“Naomba nitoe ahadi kwenu, najua kwamba kuna vijana wengi watagombea nafasi mbalimbali. Tuwahakikishie kwamba tutawashika mkono wapate nafasi hizo kwani tunapenda kuona vijana wengi bungeni na Baraza la Wawakilishi,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, wataongeza vijana wengi serikalini katika nafasi mbalimbali kwani wote waliopewa nafasi hawakuwaangusha na wamefanya kazi vizuri.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Muhamed Kawaida amesema programu hiyo inakwenda kuwaondoa vijana wazembe na wavivu ndani ya chama hicho.
“Tumechoshwa na longo longo, majungu, na matusi. Tunachokitaka ni kazi na katika kazi hiyo tunahitaji fursa ambazo tayari zimeshawekwa bayana katika sekta mbalimbali,” amesema.
Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Jokate Mwegelo amesema kutokana na chaguzi zilizopo mbeleni, serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, UVCCM wameona ipo haja kuanzisha vuguvugu hilo.
Amesema kampeni hiyo ni njia mojawapo ya kuendelea kuwapa moyo viongozi na wasiwape nafasi wapinzani kuonyesha kwamba hawana uwezo.
Ametumia jukwaa hilo kukiomba chama kutoa kipaumbele kwa vijana wenye uwezo kugombea nafasi mbalimbali katika chaguzi hizo zinazokuja siku za usoni.
“Tunaomba kuwaondoa hofu viongozi wetu kwamba vijana tupo timamu na tunatambua nafasi yetu kusaka kura za chama chetu,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Muhamed Dimwa amesema wataendelea kudumisha amani na kujibu hoja lakini wanapochokozwa wasikubali kuchokozeka.
“CCM tuendelee kuhubiri amani na kujibu hoja si vihoja, lakini tunapochokozwa tusikubali kuchokozeka,” amesema Dk Dimwa.
Kampeni hiyo kitaifa inatarajiwa kuzunguka katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.