Dk Nchimbi: Serikali ijenga makumbusho ya vita vya Kagera

Bukoba. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ameielekeza Serikali kujenga makumbusho maalumu ya vita vya Kagera vilivyopiganwa kati ya majeshi ya Tanzania na vikosi vya Idd Amin wa Uganda.

Lengo la kuwa na makumbusho hiyo, amesema ni kuhifadhi historia hiyo kwamba Tanzania iliwahi kupigana vita na adui yake na ikashinda. Pia, amesema lengo jingine ni kuieleza dunia kwamba Watanzania walikuwa wamoja wakati wa vita hivyo ilivyopigana mwaka 1978 – 1979.

Dk Nchimbi amebainisha hayo leo Agosti 10, 2024 kwenye mkutano wa hadhara ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika Mkoa wa Kagera, akikagua uhai wa chama, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na kukagua maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Dk Nchimbi amewapongeza Watanzania wote hususan wakati wa Kagera kwa kujitoa katika vita hiyo hadi walipofanikiwa kumng’oa Amin madarakani na kulinda mipaka ya Tanzania, hasa eneo la mkoa huo lililokuwa limemegwa.

“Serikali ihakikishe makumbusho ya vita kati ya Tanzania na vikosi vya Amin yanajengwa ili kulinda historia hii,” amesema Dk Nchimbi.

Amesisitiza kwamba wakati wa vita hivyo, Watanzania walionyesha umoja wa hali ya juu kwa kuchangia gharama za vita hiyo. Amesema wapo waliochangia ng’ombe, wengine walitoa vyakula na hata fedha ili kuhakikisha malengo ya nchi katika vita hivyo yanatimia.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo wa CCM, amemwelekeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki kuifanyia kazi na kupata ufumbuzi wa changamoto ya wanyama waharibifu wanaovamia makazi ya watu, kuharibu mazao na kutishia uhai wa binadamu katika Wilaya ya Karagwe.

Akiwa katika Wilaya ya Karagwe na Kyerwa, Dk Nchimbi amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu kuvamiwa na wanyamapori wanaohatarisha usalama wao na mali zao, hasa mazao yao.

Malalamiko hayo ya wanyama wakali yametokewa na wananchi katika vijiji vya Kata ya Kihanga (Kihanga, Kibwela na Mshabaiguru), ambako wamedai tembo wanavamia mashamba ya wakulima, kuharibu mazao na kuhatarisha maisha wa wananchi.

Dk Nchimbi ameagiza changamoto hiyo ishughulikiwe haraka ikiwemo kutafuta namna ya kudhibiti wanyamapori hao, ili wasiendelee kuleta madhara kwa wananchi na katika shughuli zao za kilimo.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Zainab Katimba amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuondoa changamoto kwenye sekta za afya na elimu ili kuwawezesha wanafunzi kupata huduma hizo kwenye maeneo yao.

“Serikali imetoa fedha za kutosha kwenye kila wilaya katika mkoa huu, vituo vya afya vinajengwa, shule zinajengwa kila kona na pia barabara hadi vijijini,” amesema Katimba.

Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Organaizesheni, Issa Gavu Haji amewataka wananchi wa Kagera kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ili waweze kuchagua viongozi wanaowataka uchaguzi ukifika.

“Mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa, jitokezeni kujiandikisha kwenye daftari la ukaazi na Daftari la Kudumu la Wapigakura ili mpate haki yenu ya kuchagua viongozi mnaowataka,” amesema Gavu.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts