KMC yataka Sh200 milioni Awesu acheze Simba

MWANASHERIA wa KMC ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi wa timu hiyo, Cheaf Said amesema kiungo Awesu Awesu bado ni mchezaji wao halali na Simba wakimtaka warudi mezani kwao kwa ajili ya mazungumzo wakiwa na Sh200 milioni.

Amefunguka hayo muda mchache baada ya kumalizika kwa kikao chao na Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ambapo amesema hivi sasa wanasubiri uamuzi wa kamati hiyo.

“Ni kweli Awesu aliomba kuvunja mkataba akiwa na sababu kuwa anaenda kukuza kipaji sehemu nyingine, barua hiyo aliandika Julai 10 na siku ya pili tulikaa naye kikao tukamwambia hatujakubali,”  alisema na kuongeza;

“Uamuzi wa kumkatalia ni sababu alizoleta kwa ajili ya kuvunja mkataba, alitakiwa kufanya hivyo kama timu imeshuka daraja au imeshindwa kumpa mahitaji yake, hicho kitu kwake hakipo, ni wazi kuwa amerubuniwa wa Simba ambayo inasema imemsajili akiwa mchezaji huru.”

Cheaf alisema Awesu bado ni mchezaji wao na leseni yake inasoma kwenye timu yao, huku akibainisha kwamba Simba ambao wanasema ni mchezaji wao waliwafuata siku mbili kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kuomba kibali ili wamtumie, wakawakatalia.

“Kama wamemsajili mchezaji huru kwetu walifuata nini? Msimamo wetu ni Awesu kurudi KMC na kama Simba wapo tayari kulipa kiasi cha shilingi milioni 200 tunawaachia,” alisema na kuongeza;

“Awali makubaliano yetu yalikuwa ni Simba watulipe shilingi milioni 70, walikwama kwa sababu walikuwa na shilingi milioni 60, sasa kutokana na usumbufu waliotupa tunatama shilingi milioni 200.”

Related Posts