Musoma. Mkanganyiko kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura pamoja na uandikishaji wa wapiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa umepelekea muitikio mdogo wa wapiga kura kwenye chaguzi hizo.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wametakiwa kuhakikisha wanashiriki kwenye uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura unaoendelea na kisha kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa watakapotakiwa kufanya hivyo.
Ofisa uchaguzi Manispaa ya Musoma, Deus Obure amesema wananchi wanapaswa kutambua kuwa kila uchaguzi una taratibu zake na chaguzi zote ni muhimu kwa maendeleo ya nchi, hivyo, wanapaswa kushiriki katika kila uchaguzi.
Obure ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao kazi kati ya waandishi wa habari na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru), Mkoa wa Mara, leo Agosti 10, 2024.
“Uchunguzi unaonyesha watu wakishajiandikisha na kufanya maboresho kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura wanadhani wamemaliza kila kitu, wanadhani daftari hilo lina uhusiano na upigaji kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesema Obure.
Ametolea mfano uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 ambapo kwa Manispaa ya Musoma maoteo yalikuwa ni kuandikisha wapiga kura 88,000 lakini waliojindikisha walikuwa 24,000 pekee.
“Mnaona hata nusu ya maoteo hatukufikia, Serikali iliamua kuongeza tena siku 10 za kujiandikisha, ikabidi jitihada zaidi zifanyike na idadi ikaongezeka kufikia 60, 000,” ameongeza Obure.
Obure amesema mwaka huu katika uchaguzi wa serikali za mitaa, watu wapatao 96,000 katika manispaa hiyo wanatarajiwa kuandikishwa kushiriki uchaguzi huo.
Amewataka waandishi wa habari kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki kikamilifu pamoja na kushiriki kwenye kampeni za kupinga vitendo vya rushwa.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Mohamed Shariff, amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha inazuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
“Malengo haya yatafikiwa pakiwepo ushirikiano baina ya taasisi na jamii, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, kwani lengo kuu la uchaguzi ni kuwapata viongozi bora kwa ustawi wa wananchi, kama ilivyobainishwa kwenye Katiba,” amesema Shariff.
Amesema wananchi wanapaswa kuepuka vitendo vitakavyosababishwa washindwe kuwachagua viongozi wanaofaa, ikiwa ni pamoja na kupokea rushwa za pesa taslimu, kanga, na vitu vingine.
“Vitendo vingine vinadhalilisha utu wa mtu. Hivi kweli mtu unakubali kumpigia kura mgombea asiyefaa kisa pombe, yaani mawazo yake yanaingia kwako na kufanya maamuzi anayotaka yeye kwa kununuliwa pombe. Kwanini ukubali utu wako udhalilishwe? Watanzania tubadilike, waandishi mnalo jukumu katika hili,” ameongeza Shariff.
Baadhi ya waandishi wamesema zipo sababu zingine zinazowafanya wananchi kushindwa kujitokeza kupiga kura, hivyo ni vema sababu hizo zikafanyiwa kazi ili kuruhusu watu wenye sifa za kupigakura washiriki kwenye uchaguzi.
“Tumeambiwa licha ya watu kujiandikisha kwa kusuasua kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, lakini uchaguzi ulifanyika kwenye mitaa mitano tu kati ya mitaa 79 baada ya wagombea kwenye mitaa 74 kupita bila kupingwa,” amesema Fazel Janja Janja.
Amesema suala la rushwa ni miongoni mwa vitu vinavyosababisha wengi kukata tamaa ya kupiga kura wakiamini maamuzi yao hayatapewa nafasi.
Mkazi wa Manispaa ya Musoma, Joel Sabato, amesema umefika muda wananchi waone umuhimu wa kushiriki kuchagua viongozi wanaofaa badala ya kuwa na visingizio, hali ambayo haina afya kwenye suala la demokrasia.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.