Mke aomba mumewe atangazwe marehemu

Dar es Salaam. Katika matukio nadra kutokea, hili la Stela Ishengoma, kufungua maombi Mahakama Kuu, akiiomba itamke kuwa mumewe, Dawson Ishengoma ni marehemu baada ya kutomuona kwa miaka saba mfululizo ni mojawapo.

Katika maombi hayo namba 71 ya mwaka 2023, Stella kupitia kwa wakili wake, Joseph Sungwa, alieleza kuwa mume wake huyo hajawahi kusikika au kuonwa na familia yake tangu Juni 20, 2018 na wakati anatoweka alikuwa na umri wa miaka 60.

Baada ya kusikiliza hoja za Stella, Jaji A.A Omari wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Temeke jijini Dar es Salaam alikubali maombi hayo akisema miaka mitano na saba inatosha kumtamka Dawson kuwa amekufa.

Katika uamuzi alioutoa Agosti 6, 2024 na nakala yake kupatikana kwenye tovuti ya mahakama Agosti 9, 2024, Jaji Omari amesema katika maombi hayo, Dawson hajasikika wala kuonekana tangu Juni 2018 na kufanya kuwa miaka saba.

“Katika mazingira haya na kukosekana kwa ushahidi mwingine wowote kuthibitisha tofauti, hitimisho pekee ambalo mahakama inaweza kulifikia ni kuwa Dawson Buberwa Ishengoma anaweza kuwa amekufa,” amesema Jaji Omary.

Amesema mbali na mke kuomba mumewe atamkwe marehemu, aliomba pia aruhusiwe kuanzisha mchakato wa kuomba kuwa msimamizi wa mali za marehemu na kuorodhesha mali lukuki ambazo wanamiliki pamoja naye.

Mali hizo kulingana na kiapo chake ni nyumba iliyopo Kijiji cha Ruzinga wilayani Missenyi mkoani Kagera, kiwanja chenye nyumba mbili mtaa wa Ghana jijini Mwanza na kiwanja ambacho hakijaendelezwa katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Nyingine ni viwanja vitatu katika Mtaa wa Ruchelele jijini Mwanza, eneo la machimbo ya madini lililopo Masumbwe, Kahama mkoani Shinyanga, ekari sita za ardhi Usagara jijini Mwanza na kiwanja kilichopo Mwatilole, Geita.

Katika orodha hiyo, limo eneo la machimbo ya madini Geita, kiwanja chenye nyumba mbili eneo la Buyuni, Kigamboni mkoani Dar es Salaam, ekari tano zilizopo Lugoba, Chalinze na ekari nne zenye nyumba nne, zilizoko Goba wilayani Ubungo.

Katika usikilizwaji, wakili Sungwa alisema mteja wake alikuwa ana maombi kwa mahakama kutoa amri mbili, na moja ya amri hizo ni kutamka mumewe ni marehemu baada ya kutoweka kwa miaka saba tangu mwaka 2018.

“Kwa hiyo muombaji kama mke wa Dawson Buberwa Ishengoma anaiomba mahakama hii kutumia mamlaka yake kupitia kifungu 161 cha Sheria ya Ndoa sura ya 29 RE 2019 kutamka kuwa ni marehemu,”ameeleza wakili huyo kortini.

Kulingana na wakili huyo, amri nyingine ni mteja wake kuruhusiwa kuwasilisha barua ya maombi ya kuwa msimamizi wa mirathi ya mumewe,  na kwamba Dawson wakati anatoweka alikuwa na umri wa miaka 60.

Wakili huyo alisema Dawson hajawahi kuonekana wala kusikika mahali alipo na kwamba, familia yake imejaribu mara nyingi kumtafuta kupitia matangazo katika vyombo vya habari lakini jitihada zao hazikuweza kuzaa matunda.

Kulingana na wakili huyo, muombaji alitoa taarifa ya kutoweka kwa mumewe katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Dar es Salaam na kupewa namba ya taarifa C/D/RB/4387/2018 na hakuna mafanikio yoyote ya kupatikana kwake.

Akiegemea mfano wa maombi mengine kama hayo ambayo mtu aliyetajwa kuwa Kajura alitangazwa kuwa marehemu, wakili huyo aliiomba mahakama kwa niaba ya mteja wake, kumtangaza Dawson kuwa ni marehemu.

Related Posts