TUMESHUHUDIA Dabi ya Kariakoo bora kabisa Alhamisi iliyopita. Soka lilipigwa kweli kweli pale kwa Mkapa. Hakuna aliyetaka kupoteza hata sekunde.
Licha ya ushindi wa Yanga, mpira ulikuwa mzuri sana. Ulikuwa wa ushindani na ufundi mkubwa. Uliakisi ukubwa wa soka la Tanzania kwa sasa.
Kabla ya mchezo Yanga alipewa nafasi kubwa ya kushinda. Wapo walioamini angeshinda kwa mabao mengi kutokana na Simba kuwa na wachezaji wengi wapya.
Ila ndani ya uwanja mambo yalikuwa tofauti. Simba ilikuja ikiwa imeimarika zaidi. Ilicheza kwa nidhamu kubwa. Walikuwa fiti kwa dakika zote 90.
Mechi hii imetoa taswira tofauti kabisa kwa msimu huu. Simba imesajili wachezaji wengi, ila asilimia kubwa wako vizuri.
Kipa Moussa Camara. Ndio kwanza ana wiki moja tu ndani ya timu. Ameonyesha kiwango bora. Ana utulivu mkubwa. Anatulia akiwa na mpira mguuni. Anajiamini.
Kwa kifupi Camara ameonyesha kuwa ni kipa wa kisasa. Hana papara. Anacheza vyema na mabeki wake. Anasahihisha makosa ya mabeki wake.
Wa pili ni huyu beki mpya wa kati Karaboue Chamou. Ameingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza kwa ubora mkubwa. Ana utulivu. Ana hesabu nzuri za ukabaji. Ameweza kucheza kwa maelewano na Che Fondoh Malone.
Kwa huyu beki tunaweza kusema mbadala wa Henock Inonga amepatikana haraka tofauti na watu walivyofikiria. Karaboue anaweza kucheza vyema zaidi na Malone tofauti na ilivyokuwa kwa Inonga.
Kiungo Debora Fernandez hana maswali. Anawapa Simba kile walichokosa katika safu ya ulinzi kwa muda mrefu. Anakaba vizuri. Anachezesha timu vizuri kutokea chini. Anapanda kuongeza mashambulizi.
Anafanya pia majaribio ya kufunga kwa mbali. Ni kiungo wa mpira. Amestahili jezi namba 17 aliyokuwa akivaa Clatous Chama.
Augustine Okejepha ameonyesha kuwa pacha mzuri katika kiungo akicheza na Debora. Wana maelewano mazuri. Ni kama wamecheza pamoja kwa muda mrefu.
Okejepha ana nidhamu kubwa zaidi katika kukaba. Alipoingia katika mchezo wa juzi alipunguza kabisa madhara ya Pacome Zouzoua aliyekuwa anasepa na kijiji. Akaweka utulivu mkubwa katika timu.
Kwa upande wa Joshua Mutale hakuna maswali sana. Ni winga mwenye kasi. Anapopata mpira anawaza zaidi kwenda kushambulia. Haogopi mabeki wa timu pinzani. Anajiamini. Hapa Simba imepata mtu wa maana.
Kuna baadhi ya watu wana shaka na mshambuliaji, Steven Mukwala lakini naweza kumwekea dhamana. Anaonekana ana kitu. Ana kasi pia na utulivu akiwa na mpira. Kwa aina yake ya uchezaji anaweza kuwa na madhara zaidi akicheza na straika mwingine kwa pamoja.
Jean Charles Ahoua tuendelee kusubiri makeke yake. Ila ameonyesha pia ni kiungo anayetumia akili nyingi. Hana chenga za maudhi kama Chama ila ana akili kubwa ya mpira.
Kwa kifupi, nilichokiona kwenye dabi ni kuwa Simba imefanya usajili mzuri. Ni tofauti kabisa na mwaka jana. Ni tofauti na mwaka juzi. Kuna kitu wanakipika.
Kwa upande wa Yanga wameendelea kuwa katika ubora wao. Wanacheza vyema katika maeneo yote.
Mechi ikiwa ngumu wana watu wa kuamua mechi. Ni kama walivyofunga bao la juzi. Akili ya Pacome. Akili ya Dube. Akili ya Maxi. Zilitosha kuamua mchezo. Walivuruga safu ya ulinzi ya Simba iliyokuwa na wachezaji wengi nyuma.
Kwenye safu ya ulinzi kina Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto wameendelea kuwa bora. Wanacheza vyema sana. Wanatimiza majukumu yao vizuri.
Hakuna maswali kuhusu ubora wa Yanga. Wataendelea kuwa washindani wakubwa kwenye Ligi ya ndani na Afrika.