Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemkuta na kesi ya kujibu, mwalimu wa mafunzo kwa vitendo, Frank Mpogoma anayekabiliwa na shtaka moja la kumlawiti mtoto mwenye ulemavu wa miguu.
Mpogoma anadaiwa kumlawiti mtoto huyo mwenye umri wa miaka 13, Februari 23, 2023 katika Shule ya Msingi Maweni iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Uamuzi huo umetolewa Agosti 9 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake na mahakama hiyo kupitia ushahidi wa mashahidi sita na vielelezo viwili vilivyowasilishwa.
“Mshtakiwa umekutwa na kesi ya kujibu, hivyo unatakiwa kujitetea” amesema Hakimu Swallo.
Hakimu baada ya kueleza hayo, mshtakiwa amesema atajitetea mwenyewe kwa njia ya kiapo na hatakuwa na shahidi.
Baada ya kusikiliza maelezo ya mshtakiwa, Hakimu Swallo ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 12, 2024 kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kujitetea.
Awali, Wakili wa Serikali Asiat Mzamiru, alidai kuwa Kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa upande wa mashtaka na baada ya kufunga ushahidi wao, ndipo Mpogoma alipokutwa na kesi ya kujibu.
Miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi dhidi ya mwalimu huyo, ni pamoja na Koplo Salome Kiula, kutoka Dawati la Jinsia na Watoto katika Kituo cha Polisi Kigamboni
Katika ushahidi wake Koplo Kiula, alidai mwalimu huyo wa mafunzo kwa vitendo alimlawiti mtoto huyo wakiwa darasani baada ya kumziba mdomo.
Kiula ambaye ni shahidi sita wa upande wa mashtaka alidai akiwa askari mpelelezi pia anayehusika na dawati la jinsia kituoni hapo, akiwa kwenye majukumu yake Februari 22, 2023 walifika wanawake wawili wakiwa na mtoto ambaye ni mlemavu wa miguu.
“Mmoja wa wanawake hao alijitambulisha kama Mwalimu Fatuma na mwingine ni mama mzazi wa mtoto huyo. Mwalimu Fatuma alinieleza kuwa majira ya saa moja asubuhi, akiwa shuleni Maweni, alisikia mtoto analia darasani.
“Baada ya kusikia kilio mwalimu huyo alikwenda darasani na akamkuta mtoto huyo na baada ya kumuhoji, alimweleza kuwa amelawitiwa na mshtakiwa ambaye alikuwa ni mwalimu wa mafunzo kwa vitendo shuleni hapo,” alidai.
Alieleza kuwa siku hiyo ya tukio, mtoto huyo alipelekwa shule na mama yake na kumshusha katika moja ya korido na kuingia darasani.
“Baadaye Mpogoma aliingia akiwa ameshika simu kubwa na kumuonyesha muathirika picha za ngono na kumtaka wafanye kama inavyoonesha katika picha hizo,” alidai shahidi.
Shahidi aliendelea kudai kuwa muathirika alikataa, ndipo Mpogomo alimziba mdomo na kumvua nguo ya ndani na yeye akajivua za kwake na kumlawiti.
Alidai kuwa Mwalimu Fatuma baada ya kutoa maelezo hayo katika dawati hilo, shahidi huyo aliwapa fomu namba tatu ya Polisi (PF3), waende hospitali kuthibitisha maelezo hayo.
“Tuliongozana hadi kituo cha Afya Kigamboni ambapo muathirika alifanyiwa vipimo na kuthibitika kwamba kweli alilawitiwa, tulipewa ripoti ya kitabibu na kurejea kituo cha polisi na mshtakiwa alikamatwa,” alidai shahidi.
Baada ya hapo, Kiula aliandaa jalada la uchunguzi na aliteuliwa kuwa mpelelezi wa kesi hiyo, pia aliandika maelezo ya mashahidi wote muhimu na aliendaa vielelezo.
Shahidi alidai kuwa walifanya gwaride la utambuzi na mtoto huyo alimtambua mshakiwa aliyemfanyia kitendo hicho katika gwaride hilo.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Swalo aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 12, 2024 kwa ajili ya mshtakiwa kujitetea.