Unguja. Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Profesa Joseph Msambichaka amesema uamuzi wa Serikali kujenga ofisi na maabara Zanzibar utasaidia kusogeza huduma ya upimaji wa mionzi karibu na wananchi.
Profesa Msambichaka amesema hayo Agosti 10, 2024 baada ya kutembelea ofisi na maabara za TAEC Zanzibar zilizojengwa eneo maalumu lililotengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kama eneo la viwanda ambako ujenzi wa ofisi na maabara za TAEC umekamilika kwa asilimia 100.
Amesema zamani ilibidi kubeba sampuli kutoka Zanzibar kupeleka Arusha au Dar es Salaam kwa ajili ya upimaji wa mionzi jambo ambalo liligharimu fedha nyingi na muda ili kupata majibu, kwa sasa upimaji utafanyika Zanzibar hivyo kusaidia kukuza uchumi.
“Hii ni hatua muhimu ilikuwa kazi kubwa, inatumia gharama na muda mwingi kusafirisha sampuli kwenda Tanzania Bara, lakini kwa sasa kila kitu kitaishia hapa,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania, Profesa Najati Kassim Mohamed ameishukuru Serikali kwa kutoa eneo la ujenzi wa ofisi na maabara za TAEC jambo litakalosaidia kuhakikisha matumizi salama ya mionzi nchini.
Eneo la viwanda la Dunga Zuze ni eneo maalumu lililotengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lenye ukubwa wa ekari 173 na Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ndiyo taasisi ya kwanza kujenga ofisi na maabara katika eneo hilo.
Wakati akiweka jiwe la msingi katika eneo hilo Agosti 7, 2024 Rais Hussein Mwinyi alisema eneo hilo litakuwa chachu ya kuendeleza biashara na viwanda, na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Alipongeza Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kwa ubunifu wao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Fatma Mbarouk amesema mradi huo unajumuisha ujenzi wa tangi la maji lenye lita za ujazo milioni moja, uchimbaji wa visima vitatu, usambazaji wa bomba na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 7.83.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 wizara imetenga Sh40.32 bilioni katika ujenzi wa ukuta, mabanda ya viwanda, ujenzi wa miundombinu na umeme katika eneo hilo.
Kabla ya kuanza mradi huo, wizara ililipa fidia ya vipando na majengo kwa wananchi 41 wa eneo hilo, jumla ya Sh590.7 milioni zilitumika.