Rais Samia aeleza kwa nini anajikita kuboresha kilimo

Dar es Salaam. Rais Samia Samia Suluhu Hassan ameeleza mambo matatu yalimyofanya ajikite kuboresha kilimo, huku akitoa maagizo ya fedha kutolewa kuongeza mtaji wa uanzisha benki ya ushirika.

Amesema mambo hayo kuwa ni sekta ya kilimo inawagusa zaidi wananchi wa chini, wakiwemo wanyonge na wenye hali duni; dunia kukumbukwa na tishio la kutokuwa na uhakika wa chakula na sekta hiyo kuwa na ajira kwa vijana ambao ni zaidi ya asilimia 60 ya watu.

Rais Samia ameeleza hayo Agosti 10, 2024 alipozungumza na maofisa ugani na wanaushirika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.

Pia amemwagiza Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande kwenda kulifanyia kazi ombi la kutoa asilimia 10 kwa ajili ya uanzishwaji wa benki ya ushirika, akiwapa Sh5 bilioni ili kufikia asilimia 51 ya hisa katika benki hiyo.

“Nataka kusema hizo Sh5 bilioni zipo njooni mchukue, na hii ni kwa sababu tunaharakisha benki iweze kuundwa kwa haraka iweze kufanya kazi ya vyama vya ushirika… Kwa changamoto yoyote njooni mtuone hatutaki benki hii ishindwe,” amesema.

Rais Samia amesema Afrika ndilo bara linalotegemewa kuzalisha chakula, hivyo Tanzania haina sababu ya kutokuwepo katika nchi yenye uzalishaji wa chakula ili kulilisha bara hilo na maeneo mengine ya dunia.

“Hii ni fursa tuliyoipata Tanzania kutokana na matokeo yanayotokea duniani ya kutokuwa na usalama wa chakula. Tukifanya vizuri katika kilimo, vijana watajiajiri au kuajiriwa katika maeneo ya kilimo, ndiyo maana Serikali tumeelekea katika sekta hii ambayo ndani yake kuna kilimo mazao, ufugaji na uvuvi,” amesema.

Amesema katika ziara alizofanya hivi karibuni Rukwa na Morogoro, aliwashukru wakulima kwa kuhakikisha kunakuwa uhakika na usalama wa chakula.

Rais Samia amesema watalaamu hao ni mashujaa wasioimbwa, lakini wamekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya kilimo.

“Hawa ni mashujaa wasiosemwa na mtu, lakini uhakika wa chakula tunaojivunia, asilimia 128 ya utoshelezi wa chakula Tanzania unatokana na maofisa ugani, licha ya kusahaulika, lakini ndio watalaamu wanaotuletea uhai, usalama na uhakika wa chakula,” amesema.

Amesema matokeo ya ongezeko la tija, uzalishaji na mchango wa pato la Taifa unachangiwa na juhudi za maofisa ugani.

“Niliwashukuru wakulima kwa sauti kubwa, leo nawashukuru ninyi kwa sauti kubwa pia kwa mchango wenu muhimu,” amesema.

Amesema maofisa ugani na ushirika wana jukumu kubwa la kuchochea uchumi wa Tanzania, ndiyo maana Serikali iliboresha mazingira yao ya kazi ikiwemo kuwawezesha vitendea kazi.

“Tunavyokwenda mbele nimeona matokeo chanya kwa maofisa ushirika na ugani kwenye sekta ya kilimo, hata lile la wakulima na wafugaji kukubaliana kukaa pamoja na kusema imetosha, mwanga umeonekana,” amesema.

Hata hivyo, amewataka maofisa ugani kutulia katika maeneo wanayopangiwa na Serikali ili kuwahudumia wananchi.

Amesema lengo la Serikali kwa siku za usoni ni kuhakikisha kunakuwa na ushirika unaondeshwa kisasa, uwekezaji unafanywa kitalaamu ukilenga kumnufaisha mwana ushirika, siyo kumkandamiza.

Mwakilishi wa maofisa ugani, Enock Ndunguru amesema kumekuwa na kasi kubwa ya maendeleo katika sekta ya kilimo, ikiwemo maofisa ugani kupewa vitendea kazi.

Amemwomba Rais Samia kuzitengenisha sekta za kilimo na mifugo zilizounganishwa kuwa moja katika ngazi ya serikali za mitaa, akisema inaleta shida kwenye utekelezaji wa majukumu.

Rais Samia amewataka mawaziri wa sekta husika kukaa pamoja kuangalia sheria, kuongeza au kubadilisha kwa lengo la kulifanyia kazi.

Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe amesema awali maofisa ugani wa kilimo walisahaulika, lakini sasa hali imekuwa tofauti kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali.

Amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani mwaka 2021, bajeti ya ugani ilikuwa Sh682 milioni lakini katika mwaka wa kwanza aliongeza hadi Sh17.7 bilioni.

Bashe amesema kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), watawajengea uwezo ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya kukuza sekta ya kilimo.

Amewataka maofisa ugani kutimiza wajibu wao kwa wakulima wanaowapa huduma, akihimiza uadilifu ili kuwaondoa Watanzania katika umasikini.

Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, amesema maofisa ugani ni watu muhimu waliobeba matumaini ya kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kila mkulima wanayemsaidia au shamba wanaloelimisha ili kuwa na Tanzania yenye chakula cha kutosha na uchumi imara.

“Maofisa ugani ni madereva wa mabadiliko wakichochea mchakato wa uzalishaji bora, kufufua ardhi iliyokosa rutuba na kuleta matumaini mapya kwa mamilioni ya wakulima na wafugaji,” amesema.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema maofisa ugani wa uvuvi na mifugo wamepata vitendea kazi zikiwemo pikipiki zaidi ya 1,500 zilizosambwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Pia mafunzo rejea ya teknolojia na maarifa ya kisasa yametolewa kwa maofisa ugani wa mifugo na uvuvi 3,600.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ushirika, Abdulmajid Nsekela amesema katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo walipitia baadhi ya masuala ikiwemo mali za ushirika na sheria za sekta hiyo.

“Ushirika wana mali nyingi lakini huenda hawazifahamu au haziko katika vitabu halisia, lakini tulifanya kazi ya kuzikagua mali za vyama vya ushirika 610 zenye thamani ya Sh4.2 trilioni,” amesema.

Related Posts