Serikali yahamisha mali za Kiwanda cha Chai Mponde

Dodoma. Uwekezaji wa Sh4.05 bilioni utakaofanywa na Serikali katika Kiwanda cha Chai cha Mponde kilichopo mkoani Tanga, unatarajiwa kutoa soko kwa wakulima kwa kuchakata majani kilo milioni 5.8 kwa mwaka.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Agosti 9, 2024 na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu wakati wa kusaini mkataba  wa wanahisa na mikataba ya uhamishaji wa mali pamoja na hati ya makabidhiano ya mali.

Kiwanda hicho sasa kinamilikiwa na Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa asilimia 42 za hisa, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao wana hisa ya asilimia 42 na Msajili wa Hazina kwa asilimia 16.

Kiwanda hicho kilikabidhiwa kwa wanahisa hao ambao wameunda Kampuni ya Mponde Holding Company Limited (MHCL), baada Serikali kuvunja mkataba kati yake na Wakulima Wadogo wa Chai (UTEGA) kwa sababu mwekezaji aliyepewa kiwanda hicho alishindwa kulipa kiasi chote cha mauzo cha Sh750 milioni.

Akizungumza Mchechu amesema tangu kiwanda hicho kianze uzalishaji chini ya wabia hao wapya, kimesindika kilo 501,271 za majani mabichi ambayo yalitoa chai iliyotengenezwa kilo 100,244.

Amesema kampuni ya MHCL ambayo wanahisa wamewekeza tayari Sh2.5 bilioni na imeuza kilo 93,488 za chai iliyotengenezwa ambayo ilizalisha Sh201.8 milioni.

“Kiwanda kinategemea masoko ya ndani na nje ya nchi, ambapo hadi sasa kilo 24,460 zimeishauzwa na tani 50.  Kiwanda kinategemea kuajiri watu 79 za kudumu na ajira za muda 100 hadi 300 kutegemea na msimu wa mavuno,” amesema.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathimini wa Mashirika yasiyofanya Biashara katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Emanuel Luvanda amesema kiwanda hicho kinakwenda kutengeneza soko kwa wakulima wadogo hususani walio katika maeneo ya Wilaya za Lushoto na Korogwe.

Amesema miongoni mwa mali zilizokabidhiwa kwa wamiliki hao ni pamoja na nyumba 12 za makazi zilizo nje ya eneo la kiwanda ambazo hapo awali zilikuwa zilitumiwa na maofisa ugani pamoja mashamba manne ya miti.

“Pamoja na mkataba huo pia tumeandaa mkataba wa uhamishaji mali ambao unahamisha mali zote zisizohamishika na zinazohamishika,” amesema.

Amesema mkataba huo unahusika pia na haki ya kutumia msitu wa Sakare, mali zote zilizopo katika eneo la kiwanda hicho kuanzia siku ya kurejesha kwa Kiwanda Serikalini, hakimiliki na mali nyingine zozote zinazohusiana na kiwanda.

Makabidhiano ya kiwanda hicho yalifanywa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF John Mduma, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru na Mchechu.

Related Posts