St. Patrick Academy yabeba kombe la mashindano ya ‘Champion of Tomorrow’

Na Mwandishi wetu, Arusha

HATIMAYE timu ya soka ya mpira wa miguu ya sekondari ya St Patrick Academy imekuwa bingwa wa mashindano ya ‘Champion of Tomorrow’ baada ya kuichapa sekondari ya Sombetini kwa goli 4-1 katika fainali iliyochezwa jana kwenye uwanja wa Shule ya Kimataifa ya UWC Arusha.

Iliwachukua dakika 6 tu za mchezo huo kwa St. Patrick kupata goli lake la kwanza la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji wake hatari, Ramadhani Juma baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa timu ya soka ya sekondari ya Sombetini.

Katika dakika ya 26, Sekondari ya Sombetini ilisawazisha goli hilo kupitia kwa mshambuliaji wake Yusuf Kassim aliyepata pasi nzuri kutoka kwa Rashid Omari aliyepiga chenga mabeki wa timu soka ya St.Patrick na kutoa pasi hiyo iliyozaa goli.

Wakicheza kwa kasi kubwa, St.Patrick Academy kupitia tena kwa mshambuliaji wake Ramadhani Juma iliongeza goli la pili katika dakika ya 35 baada ya kufunga goli zuri kupitia mpira wa kona iliyoingia moja kwa moja katika goli la timu soka ya Sombetini na kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa goli 2-1.

Ramadhani Juma aliendelea kuwa mwiba kwa timu ya soka ya sekondari ya Sombetini baada ya dakika ya 66, kuongeza goli la tatu kupitia mpira wa adhabu ndogo alioupiga na kuingia golini kwa Sombetini moja kwa moja. Ramadhani Abbasi alihitimisha kapu la magoli kwa timu yake ya St.Patrick kwa kufunga goli la nne dakika ya 79 ya mchezo.

Mara baada ya mchezo huo, muandaaji wake, Ashok Mittal alizipongeza timu zote mbili kwa mchezo mzuri walioonyesha tangu ufunguzi wa mashindano hayo Agosti Mosi, 2024 ambapo timu hizo hizo zilikutana na kutoka sare na goli 2-2.

Ashok akiambatana na mgeni maalum Mbunge wa jimbo la Arusha, Mrisho Gambo, waliwagawia washindi wa pili timu ya soka ya Sekondari ya Sombetini mipira saba huku bingwa wa mashindano hayo Sekondari ya St.Patrick Academy ikizawadiwa mipira nane, kombe pamoja na medali.

Gambo amempongeza Ashok kwa ubunifu alioonyesha wa kuandaa mashindano hayo na kutoa wito kwa mamlaka zinazosimamia soka nchini ikiwemo TFF kutumia michezo hiyo kutafuta wachezaji wenye vipaji ili kuviendeleza na kuwa hazina kwa timu zetu za Taifa.

Mmoja wa wadhamini wa mashindano hayo, Mkurugenzi wa kampuni ya Mount Meru Petroleum, Atul Mittal amewapongeza wachezaji wa timu zote mbili na kuwataka kufanyia masahihisho makosa madogo madogo ambayo wamekuwa wakiyaonyesha uwanjani ili kuwafanya kuwa bora zaidi.

“Nawapongeza kwa mchezo mzuri sana ambao mmeweza kuuonyesha katika fainali hii, lakini mnaweza kuniambia mlifanyawapi makosa yenu? hasa katika dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza hadi dakika ya 66?….mkifanyia mazoezi makosa hayo, mkayarekebisha hakika nyie ni wachezaji wazuri sana na mtafika mbali,”alihoji Atul akiwa anazungumza na timu ya soka ya St.Patrick.

Mashindano hayo yalishirikisha timu nane za shule za Sekondari za Serikali na binafsi zenye mchepuo wa kiingereza ambazo ni Sekondari za St.Patrick Academy, Kilimanjaro Boys Academy, Brainy Heroes, Renea, Sombetini, Lemara, Sinon, na Mateves.
Ashok Mittal muandaaji wa mashindano ya champion of Tomorrow’ akimkabidhi nahodha wa timu soka ya Sekondari ya St. Patrick kikombe baada ya kuibuka washindi katika fainali iliyowakutanisha na Sekondari ya Sombetini

Related Posts