Taknolojia ilivyopaisha faida Mfuko wa Faida

Dar es Salaam. Mfuko wa Uwekezaji wa Faida Fund umeripoti ongezeko la faida kwa wawekezaji, kutoka asilimia 10 ya Juni 20, 2023, hadi asilimia 12 kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2024.

Hayo yamebainishwa Agosti 10, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Abdul-Razaq Badru, katika mkutano mkuu wa kwanza tangu kuanzishwa kwa mfuko huo.

Badru amesema faida hiyo inaendana na maendeleo ya soko la fedha na ni kubwa kuliko kigezo linganifu cha asilimia 9.7.

 Thamani halisi ya mfuko imeongezeka hadi Sh25.6 bilioni Juni 2024, kutoka Sh15.6 bilioni Juni 2023. Pia, idadi ya wawekezaji pia imeongezeka kwa asilimia 58, kutoka 2,041 mwaka 2023 hadi 4,806 Juni 2024.

“Ongezeko hilo limechangiwa na matumizi ya teknolojia katika kufanya miamala ya uwekezaji, kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji nchini, na elimu inayoendelea kutolewa juu ya faida zinazopatikana kupitia mifuko ya uwekezaji,” amesema Badru.

Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment (WHI), Dk Fred Msemwa amesema mfuko huo ulianzishwa na kiasi cha Sh12 bilioni na sasa una thamani ya Sh27 bilioni.

Thamani ya vipande viliuzwa kwa Sh100 wakati unaanzishwa na sasa vinauzwa kwa Sh117, sawa na ukuaji wa asilimia 17.

Kwa mujibu wa Msemwa, matumizi ya teknolojia, kama Mfumo wa Malipo ya Serikali (GEPG), yamechangia kufanikisha ukuaji huo.

Wawekezaji sasa wanaweza kujaza fomu na kuchota faida mtandaoni bila kufika ofisini.

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daud, amesisitiza umuhimu wa elimu ya fedha, akieleza kuwa watu wengi hawajawahi kuwekeza kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya fedha.

Ametoa wito kwa menejimenti ya mfuko kuwekeza katika utoaji wa elimu ya fedha ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uwekezaji.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts