Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimelaani ongezeko la matukio ya utekaji na watu kupotea nchini kikitoa orodha ya watu 83 waliofikwa na kadhia hiyo.
Mbali ya hayo, TLS imemshauri Rais Samia Suluhu Hassan mambo matatu, ikiwemo kuunda tume kuchunguza ushiriki wa Jeshi la Polisi kwenye matukio ya utekaji.
Kwa mujibu wa TLS, Jeshi la Polisi limekuwa likituhumiwa kushiriki katika vitendo vya utekaji, tuhuma ambazo limekuwa linazika mara kadhaa.
Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia taarifa na orodha ya TLS, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Camillius Wambura simu yake ya mkononi ilipokewa na msaidizi wake aliyesema IGP yupo kwenye kikao, atakapomaliza angemtafuta mwandishi wa habari.
Licha ya kusubiri na hata alipotafutwa mara nyingine simu yake haikupokewa tena.
Hata hivyo, Julai 15, 2024 akiwa mkoani Simiyu, IGP Wambura alisema Jeshi la Polisi halihusiki na vitendo vya utekaji.
Alisema ni kweli matukio ya utekaji na watu kujiteka yapo lakini Polisi wanapambana kuwakamata wahalifu na kuwaokoa wanaotekwa.
“Hatuhusiki na utekaji watu, sisi ni jeshi ambalo linalinda usalama wa watu na mali zao, wanaoleta tuhuma za namna hiyo ni vitendo vya kutuvunjia adabu, matukio ya utekaji yaliyofanyika Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa na kuwakamata wahalifu na kuwaokoa wale waliotekwa,” alisema IGP Wambura.
Mwananchi lilipomtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, simu yake haikupokewa na hata alipotumiwa ujumbe kwa mtandao wa WhatsApp ulionyesha kusomwa lakini haukujibiwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Naibu Waziri, Daniel Sillo kwa nyakati tofauti walipotafutwa simu zao ziliita pasipo kupokewa.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ally Gugu alipotafutwa alipokea simu na kueleza yupo eneo lisilo na utulivu, hivyo angerejea kuzungumza na mwandishi.
Baada ya muda kupita alipotafutwa simu iliita bila kupokelewa.
Hata alipotafutwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai alisema yupo kwenye eneo la kelele.
Alipotafutwa tena na kutumiwa ujumbe aliahidi atamtafuta mwandishi baadaye.
Pamoja na ahadi, hiyo alipopigiwa tena simu haikupokewa.
Hali ilikuwa vivyo hivyo kwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba ambaye simu yake iliita pasipo kupokewa.
TLS katika taarifa kwa umma ya Agosti 9, 2024 iliyosainiwa na Rais wa chama hicho, Boniface Mwabukusi imependekeza kuundwa chombo maalumu cha kudumu cha kuangalia utendaji wa vyombo vya dola ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na sheria.
TLS imemshauri Rais Samia kuunda tume maalumu kuchunguza matukio yote ya kupotea kwa watu, kutekwa na kuteswa, ikisema tangu mwaka 2016 hadi 2024 watu 83 wamepotea, kutekwa na wapo waliopatikana wakiwa na majeraha, huku wengine wakiwa hawajapatikana hadi sasa.
Baraza la Uongozi la TLS kupitia taarifa hiyo limesema chama hicho kinaendelea kufuatilia matukio hayo kwa ukaribu na kiko tayari kushirikiana na vyombo vyote vya dola katika kuhakikisha wahusika wote wa matukio hayo wanafikishwa katika vyombo mahususi vya haki ili haki ionekane inatendeka.
“Hata hivyo, tunatoa rai kwa Watanzania wote kuwa makini wakati wote na kutokubali kuitwa au kukutana na watu wasiowajua au kwenda mahali wasipopajua na ikibidi sana wawasiliane na wakili yeyote kabla ya kukutana au kwenda mahali wasipopajua,” imesema taarifa ya TLS.
Kutokana na taarifa ya TLS, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) kwa nyakati tofauti wamesema mapendekezo ya chama hicho ndiyo kilio chao cha muda mrefu, wakidai matukio yanayohusishwa na Jeshi la Polisi hayawezi kuchunguzwa na Jeshi hilohilo.
Utendaji wa Jeshi la Polisi pia ulizungumziwa na Tume ya Haki Jinai mwaka 2023 chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mohamed Othman Chande ikipendekeza katika ripoti iliyowasilishwa kwa Rais Samia, kuwa jeshi hilo lifanyiwe tathmini ya kina ili kulifanyia maboresha makubwa ili kuondoa kasoro za kiutendaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema mapendekezo ya TLS nao wamekuwa wakiyapendekeza hasa uwepo wa chombo mahususi cha kuangalia utendaji wa vyombo vya dola, kwani katika mataifa mengine kinakuwepo kikatiba na kinakuwa huru.
“Mtu anapopotea na polisi ndiyo wanatuhumiwa, nani ataichunguza polisi, hakuna. Hivyo hakutakuwa na uwajibikaji, kauli ya TLS ni nzuri,” amesema.
Henga amesema tamko la TLS linaonyesha namna chama hicho kinavyorejea kwenye misingi yake ya kuisaidia nchi kwenye masuala ya kisheria.
Kwa upande wake, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema wanaliunga mkono tamko la TLS.
“Kimsingi yaliyosemwa na TLS ndiyo mambo ambayo nasi tumekuwa tukishauri, tunawashukuru nao kwa kulibeba jukumu hili,” amesema.
Olengurumwa amesema matukio ya utekaji na kupotea watu nchini ni mengi kuanzia mwaka 2019 mpaka sasa takwimu walizonazo zikionyesha takribani watu 200, wakiwamo watoto.
Amesema kinachowashangaza ripoti za polisi kwa mwaka jana hazijaweka matukio ya utekaji badala yake wanaweka matukio ya watoto kupotea akihoji sababu ya matukio hayo kufichwa.
Kwa miaka ya nyuma, Olengurumwa amesema polisi walikuwa wakitoa taarifa za watu kutekwa lakini sasa wamekuwa wakizificha, hivyo jeshi hilo haliwezi kujichunguza, ndiyo maana mapendekezo yanayotolewa ni uwepo wa chombo huru cha kulichunguza.
“Yapo matukio ya utekaji hufanywa na wananchi kwa wananchi na haya polisi hawahusiki. Utekaji mwingine ni ule unaohusisha vyombo vya dola,” amesema.
Matukio yanayotajwa kufanywa na vyombo vya dola, Olengurumwa amedai ni kutekwa kwa wanahabari, wanaharakati, wanasiasa na wafanyabiashara.
“Polisi wanatuhumiwa, kwa nini Serikali haitaki kuelewa hilo, si utekaji tu hata rushwa, ukatili na watu kufia kwenye vituo ni lazima tuwe na chombo cha kulichunguza jeshi hili,” amesema.
Rejea ya baadhi ya matukio yaliyotajwa na TLS yakihusisha utekaji na watu kupotea ni tukio la mkazi wa Kigoma, Lilenga Lilenga aliyetekwa Mei 11, 2024, Donald Mboya mkazi wa Kagera aliyetoweka Juni 24, 2024 na kutopatikana hadi sasa.
Tukio lingine ni la Baraka Majiggeh aliyetoweka Juni 5, 2024, Dar es Salaam na Edger Mwakabela aliyetekwa Juni 23 Dar es Salaam na kupatikana Juni 27, 2024 mkoani Katavi akiwa na majeraha.
Chama hicho cha wanatalamu wa sheria kimesema kinasikitishwa na Jeshi la Polisi kikieleza:
“Mara kwa mara Jeshi la Polisi limekuwa likikanusha kutokea kwa matukio hayo lakini baadaye inakuja kubainika kwamba baadhi ya matukio hayo ni ya kweli.
“Mara nyingine polisi wamekuwa wakiwakamata raia wema wanaotoa taarifa hizo kwa kile kinachosemekana kusambaza taarifa za uongo, badala ya kuzifanyia kazi taarifa hizo kwa mujibu wa Katiba na sheria zinazowapasa kufanya wajibu wao wa kulinda watu na mali zao,” imesema taarifa ya TLS.
Uwepo wa matukio ya utekaji, TLS imesema ni kinyume cha ibara ya 13 (6) (e) na 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba ya kimataifa inayozungumzia haki za binadamu na inayozuia uteswaji wa watu.
Ili kutimiza matakwa ya kisheria, TLS imelitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi yake kwa weledi kwa mujibu wa Katiba na sheria ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa wananchi na mali zao unaimarika.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.