NA WILLIUM PAUL, SAME.
VIJANA takribani 62 kati yao wakiume 52 na wakike 10 wamekita kambi Tarafa ya Gonja Kata ya Bombo wilayani Same mkoani Kilimanjaro (Kikosi cha 28-24/25) kwa majuma 18 kupata mafunzo ya awali ya jeshi la akiba (Mgambo) kwa mwaka 2024.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni ambapo amewapongeza vijana hao kwa uzalendo waliouonesha kujitoa kwa moyo mmoja kujiunga na mafunzo hayo ambapo amewasisitiza pia kuwa kitendo walichokifanya ni sehemu mojawapo ya vijana kuweza kujiunga na majeshi ya ulinzi na usalama ya nchi kwani jeshi la akiba nchini Tanzania linatambulika kisheria.
“Sehemu yoyote yenye amani basi panahitajika vijana wazalendo wenye kuimarisha ulinzi na usalama wa maeneo yao ni imani yetu sasa baada ya mafunzo haya vijana wangu mtaenda kuungana na majeshi mengine kuimarisha ulinzi na usalama wa wilaya yetu” Alisema Kasilda.
Aidha ameonya pia tabia ya baadhi ya wanasiasa kuingiza itikadi zao kwenye jambo hilo na kuwakatisha tamaa baadhi ya vijana ambao walikuwa na nia ya kujiunga na mafunzo hayo, ambapo amesisitiza jambo hilo haliko sawa na kuwaomba kuacha mara moja na kutoa wito kwa vijana hao wanaodaiwa kukatishwa tamaa kufika kambini hapo kujiunga na wenzao kuendelea kupata mafunzo.
Hata hivyo kwa kipindi cha mwaka jana 2023 eilaya ya Same kuna vijana 14 waliyotokana na Mgambo ambao tayari wamejiunga na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) .