Mnamo Agosti 9 mwaka 1999, Vladimir Putin aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Shirikisho la Urusi. Na mwishoni mwa miaka ya 1999, alichukua nafasi ya Rais Boris Yeltsin aliyekuwa mgonjwa.
Mara tu alipoingia madarakani, Putin alisema kuwa Urusi ilikuwa na ingesalia kuwa nguvu kubwa. Barani Ulaya Putin anachukuliwa zaidi kama mwanamageuzi ambaye anajaribu kuijenga upya Urusi ambayo ilikabiliwa na misukosuko mnamo miaka ya 1990.
Tangu alipoingia madarakani, Putin amekuwa akiiongoza Urusi kwa mkono wa chuma. Ili kuepuka vikwazo vya katiba ya nchi hiyo, Putin alimuweka madarakani Dmitry Medvedev aliyehudumu kama rais wa Urusi kwa muhula mmoja kuanzia mwaka 2008 hadi 2012. Putin badala yake alikuwa waziri mkuu lakini aliendelea kuiongoza Urusi nyuma ya pazia.
Soma pia: NATO yajadili utayari wake wa silaha zake za nyuklia
Kwa miaka ishirini na mitano iliyopita, viongozi mbali wa Ulaya na duniani hupishana madarakani na kumkuta Vladimir Putin akiwa bado imara huku akiibadilisha Urusi kuwa “utawala wa kiimla wenye nguvu zaidi ulimwenguni,” kama alivyoeleza mtaalam wa masuala ya siasa wa Urusi Mikhail Komin.
Komin ameiambia DW kwamba hilo limewezekana kwa sababu katika robo karne ambayo amekuwa madarakani, Putin ameendelea kudhoofisha taasisi zote za kiutawala, kisiasa na kisheria za Urusi kwanza kwa kuyapokonya majimbo yote uhuru wa kuendesha mambo yao, kuvunja uwezo wa Mahakama na kuanzisha kamandi moja ya udhibiti kamili iliyo chini ya mamlaka yake.
Mbinu zingine anazozitumia Putin kusalia madarakani
Mtaalam mwingine wa siasa za Urusi anaishi Finland Grigory Nishnikov, amesema hiyo si sababu pekee iliyomuwezesha Putin kusalia madarakani. Anasema kumekuwa na matukio mengi katika kipindi cha miaka 25 ambayo yangeliweza kuwa hatari kwa utawala Putin.
Miongoni mwa matukio hayo ni maandamano katika uwanja wa Bolotnaya wa Moscow kufuatia uchaguzi wa bunge wa 2011, hatari ya kukosekana kwa utulivu baada ya unyakuzi wa rasi ya Crimea mwaka wa 2014 , machafuko yaliyofuatia mageuzi ya pensheni yenye utata mwaka 2018, maandamano makubwa ya kumuunga mkono mkosoaji wa Kremlin Alexei Navalny kote Urusi katika miaka michache iliyofuata, kuanza kwa vita nchini Ukraine mwaka 2022, ikifuatiwa na maandamano katika mitaa ya Moscow na St Petersburg.
Lakini, matukio yote yaliyodhihirisha upinzani yalizimwa kwa ukandamizaji mkubwa na vinara wa vuguvugu hilo waliuawa au kuwekwa jela. Kwa sababu hiyo, Nishnikov haamini kuwa kuna mtu aliyesalia kwa sasa ambaye anaweza kukabiliana na Putin nchini Urusi.
Mahusiano ya Putin na mataifa ya Magharibi hayakuwa mabaya wakati wote
Mnamo Juni mwaka 2001, Rais wa Marekani wakati huo George W. Bush alimtaja Putin kuwa “mwaminifu na mwenye msimamo” baada ya mkutano wao wa kilele. Miezi mitatu baadaye, alipolihutubia Bunge la Ujerumani la Bundestag, Putin alielezea uwezekano wa ushirikiano wa usalama kati ya Urusi na Ulaya na akasema haondoi uwezekano wa Urusi kujiunga na NATO na hata Umoja wa Ulaya, lakini akatilia shaka jukumu la Marekani.
Wakati huo, Umoja wa Ulaya na Urusi zilikubaliana juu ya mipango kadhaa ya ushirikiano wa kimkakati. NATO ilifungua ofisi mjini Moscow na Urusi ikawa na uwakilishi katika Jumuiya ya NATO mjini Brussels. Baraza maalum la NATO-Urusi likaundwa na likawa na jukumu ya kujadili namna mataifa ya Ulaya ya Kati na Mashariki yanaweza kujiunga kwa hiari kwenye muungano huo.
Soma pia: SIPRI: Vichwa zaidi vya nyuklia vinawekwa katika hali ya tahadhari
Ikiwa mmoja wa wasambazaji wakuu wa mafuta na gesi kwa Ulaya, Urusi ilifanya biashara nzuri na mataifa ya bara hilo. Kansela wa Ujerumani wakati huo Gerhard Schröder alimtaja Putin kuwa “mwanademokrasia asiye na dosari”, licha ya vitendo kadhaa vya ukandamizaji dhidi ya upinzani na kuminya uhuru wa vyombo vya habari nchini Urusi. Baada ya muhula wake wa uongozi, Schröder alipata nyadhifa nono katika makampuni ya nishati yanayomilikiwa na serikali ya Urusi.
Je, Utawala wa Putin uko tayari kutumia silaha zake za nyuklia?
Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine February 24 mwaka 2022, Rais Vladimir Putin na viongozi wengine wa Kremlin wamekuwa mara kadhaa wakizitishia nchi za Magharibi kwamba wanaweza kutumia silaha zao za nyuklia. Lakini je, vitisho hivyo vina uzito kiasi gani?
Siku ya kwanza ya vita, Putin alisema kuwa yeyote atakayejaribu kuwazuia au kusababisha vitisho kwa Urusi na watu wake, basi wangelikabiliwa na majibu makali na ya haraka ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia.
Kwa sasa ikiwa ni karibu miaka miwili na nusu ya mapigano, nchi za magharibi zimeipatia Ukraine mabilioni ya dola ya misaada pamoja na za silaha zenye ufanisi wa hali ya juu, ambazo baadhi yake zimetumiwa kushambulia hadi ndani ya Urusi.
Licha ya vitisho vya Kremlin kuongezeka na hata kuchukua hatua ya kupelekwa kwa silaha za nyuklia karibu na uwanja wa mapambano mpakani mwa Ukraine huko Belarus, hadi sasa Moscow imekuwa ikitoa tu vitisho hewa.
Je, ni kipi kinachoweza kusababisha mashambulizi ya nyuklia?
Alipoulizwa hilo mwezi Juni mwaka huu na mashirika ya habari ya kimataifa, Putin alisema jibu linapatikana katika kile kinachofahamika kama “fundisho la nyuklia la Urusi”, na kusisitiza kuwa nyaraka hizo zimeweka wazi kwamba
ikiwa vitendo vya mtu vinatishia uhuru na uhalali wa eneo la Urusi, basi kuna uwezekano wa Moscow kutumia zana zote ilizonazo.
Soma pia: Mahusiano ya Urusi,China kuleta utulivu wa kimataifa?
Kwa sasa vigogo wa Urusi wanamuhimiza rais abadilishe vifungu vya nyaraka hiyo muhimu kwa kupunguza vizingiti vinavyozuia matumizi ya silaha za nyuklia, na Putin tayari ameahidi kuifanyia mabadiliko hati hiyo hasa kwa kuzingatia hali ya sasa ya kimataifa. Urusi imesisitiza mara kwa mara kuwa iko tayari kutumia silaha za nyuklia ikiwa usalama wa taifa hilo utakuwa hatarini.
Je, unazifahamu nyaraka za “Fundisho la nyuklia” la Urusi ?
Nyaraka hizo zinazojulikana rasmi kama “Kanuni za Msingi na Sera ya Nchi kuhusu Nyuklia”, ilitiwa saini na Putin mnamo mwaka 2020 na inaelezea ni wakati gani Urusi inaweza kutumia silaha zake za atomiki, ambazo ni kubwa zaidi ulimwenguni.
Hati hizo zinaeleza wazi kuwa silaha za nyuklia zipo kwa ajili ya “ulinzi na kutoa onyo” ili adui yeyote afahamu kuwa majibu makali hayaepukiki ikiwa ataishambulia Urusi au washirika wake.
Soma pia: Rais Putin anasema vikosi vya nyuklia ‘daima’ viko macho
Lakini inasisitiza kuwa matumizi ya silaha hizo za nyuklia yanawezekana ikiwa tu Urusi “italazimika pakubwa,” huku ikiweka wazi kwamba Urusi inachukua hatua zote muhimu ili kupunguza tishio la nyuklia na kuzuia kuzidisha uhasama kwenye mahusiano baina ya mataifa ambao unaweza kusababisha migogoro ya kijeshi, ikiwa ni pamoja na ile ya nyuklia.
Je, kuna shambulio lolote hadi sasa ambalo limekaribia kuvuka kizingiti hiki?
Wakati Urusi ilipofanya mashambulizi makubwa katika sehemu za kaskazini mashariki mwa Ukraine karibu na mji wa Kharkiv, Washington iliiruhusu Kyiv kutumia silaha za masafa marefu ilizopewa na Marekani ili kushambulia maeneo ya Urusi yaliyopo mpakani. Lakini mashambulizi hayo hayakuweza kuchukuliwa kama tishio kwa Urusi hadi kutumia silaha zake za nyuklia.
Soma pia: Putin aamuru mazoezi ya silaha za nyuklia karibu na Ukraine
Hata hivyo, vigogo huko Moscow wamesema kuwa mfululizo wa mashambulizi ya Ukraine kwenye vituo vya jeshi la anga vinavyohifadhi makombora ya nyuklia ya masafa marefu, yanaweza kuzingatiwa kama matukio yanayoruhusu kabisa matumizi ya silaha za nyuklia kama ilivyoelezwa katika nyaraka ya “fundisho la nyuklia”.
Wafuatiliaji na wachambuzi wanahofia kuwa ikiwa Ukraine itaendelea kushambulia maeneo nyeti na ya kimkakati ya Urusi, basi Moscow katika hali ya sintofahamu inaweza pia kuanzisha mashambulizi ya nyuklia ambayo bila shaka yataishirikisha moja kwa moja Jumuiya ya Kujihami ya NATO na hivyo kusababisha vita kubwa vya nyuklia ambavyo vitakuwa na madhara makubwa.
(Chanzo: DW, AP)