Waathirika maporomoko ya tope Mlima Kawetere wakataa eneo walilotengewa

Mbeya. Waathirika 16 wa maporomoko ya tope katika Mlima Kawetele, Kata ya Itezi, jijini Mbeya wamegomea kujenga makazi kwenye viwanja walivyopewa na halmashauri.

Wamesema sababu ni kuwa maeneo hayo yako ndani ya mita 60 za hifadhi ya mto, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao na kinyume cha sheria.

Sababu nyingine zilizotajwa ni kukosekana kwa makazi ya watu karibu, na huduma muhimu kama shule, afya, maji, umeme, na miundombinu rafiki ya barabara.

Hatua hiyo imepelekea Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, kuingilia kati na kuomba Serikali kuwapimia viwanja vingine waathirika 11 kati ya 16, huku watano wakibaki kwenye eneo lililopimwa awali.

Akizungumza na Mwananchi Agosti 9, 2024, mwakilishi wa waathirika hao, Shadrack Elias, amesema ni jambo la kushangaza kwamba baada ya agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya kupatiwa viwanja, wamepelekwa maeneo yasiyo salama.

“Kimsingi, hatuko tayari kujenga katika eneo hilo kwani mazingira yake sio rafiki kiusalama na lipo ndani ya mita 60 za hifadhi ya mto na maporomoko makali, hali ambayo inatishia usalama wa maisha yetu,” alisema Elias.

Aliongeza kuwa wanaiomba Serikali itekeleze agizo la kiongozi mkuu wa nchi kwa kuwapatia maeneo rafiki na sio kuwatupa kama wanyama.

“Tunaomba Serikali kupitia kwa mbunge wetu, Dk Tulia ituangalie. Wananchi wa kipato cha chini hatuwezi kutumia nguvu kubwa kupasua mawe ya miamba kwenye viwanja tulivyopewa kwani tunajuana hali zetu kiuchumi ni duni,” alisisitiza.

Mkazi mwingine, Flora Paulo, pia alisema hawako tayari kujenga katika eneo hilo kwa sababu sio rafiki kwa usalama wao, hususan katika kipindi cha mvua nyingi.

“Jamani na sisi ni binadamu, hatuko tayari kujenga huko. Licha ya Serikali kutusaidia kwa hali na mali, tunaomba tupimiwe viwanja katika eneo lingine rafiki ambalo liko jirani na huduma za kijamii,” alisema.

Nazaret Zabron kwa upande wake ameomba Halmashauri ya Jiji itumie busara na kukuwa wao watasubiri kauli ya mwisho ya Serikali kuhusu hatima yao na si kujenga katika eneo lililotengwa.

Kufuatia kauli hizo, Mbunge Dk Tulia amesema amefika katika Kata ya Itezi kuwasikiliza wananchi na kumaliza mgogoro.

Ameeleza kwamba baada ya kuona ramani ya maeneo yaliyotengwa, ametoa maelekezo kuwa kati ya waathirika 16, watano watabaki katika eneo lililopimwa na 11 watatafutiwa viwanja vingine.

Dk Tulia amesema Serikali inawajali na itaendelea kuwafuatilia kujua hatima yao baada ya Rais Samia kutoa maelekezo kufuatia janga na maporomoko ya tope yaliyotokana na mvua nyingi msimu uliopita.

“Sio kila changamoto wananchi wanapewa viwanja, ni kutokana na athari iliyojitokeza na ndio maana Rais aliagiza mpewe viwanja, lakini baada ya kusikia maoni yenu ya kutoridhishwa na viwanja mlivyopimiwa, nimekuja kuwasikiliza,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Serikali iko pamoja nanyi. Maporomoko yalitokea muda mrefu lakini bado tunaendelea kuwafuatilia. Tumeona maoni yenu na kubaini kulikuwa na changamoto ambazo tumeweka sawa kwa kushirikiana na wataalamu wa Jiji,” amesema.

Wakati huo huo, Dk Tulia amewakabidhi Sh25 milioni zilizotolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake CCM (UWT), Mary Chatanda, kuchangia ujenzi wa makazi, huku kila mmoja akikabidhiwa kiasi cha Sh1.5 milioni.

Ofisa Mipango Miji wa Jiji la Mbeya, Dickley Nyatu, amesema viwanja 16 vya waathirika wa tope kutoka Mlima Kawetere vilipimwa na atafuatilia kujiridhisha kama eneo hilo liko ndani ya mita 60 za hifadhi ya mto.

Maporomoko hayo yalitokea Aprili 14 mwaka huu majira ya alfajiri, ambapo Mlima Kawetere ulimeguka na kusababisha nyumba 20, ikiwemo Shule ya Msingi ya Generation, kufukiwa na tope. 

Mbali na athari hizo, nyumba na mali za ndani, ikiwemo mifugo, vilisombwa na maporomoko na kusababisha zaidi ya wananchi 50 kukosa makazi.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts