HII utaipenda na mtasema mlikujaje. Ndivyo unavyoweza kusema wakati fainali ya mechi za Ngao ya Jamii itakapopigwa kesho Jumapili. Ndio, ni bonge la mechi kwa mashabiki wa soka nchini. Achana na Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Alhamisi. Achana na matokeo ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata Yanga mbele ya Simba. Achana na madudu yaliyofanywa na waamuzi wa pambano hilo. Leo kuna uhondo mwingine katika mechi hiyo ya kisasi kwa timu hizo mbili zilizomaliza nafasi mbili za juu za Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Timu hizo mbili ndizo zilizofunga kalenda ya mashindano kwa msimu uliopita kwa pambano la fainali ya Kombe la Shirikisho lililopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja.
Sahau matokeo ya mechi hiyo iliyopita ambapo Azam ilipasuka kwa penalti 6-5 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu, leo kuna mechi ya kisasi.
Hapa chini ni baadhi ya dondoo kuonyesha hii ni mechi ya kisasi na mwenye kuzichanga karata vyema ndiye atakayebeba Ngao ya Jamii kwa msimu huu ambao haina mtu kwa sasa baada ya watetezi Simba kupoteza mechi ya nusu fainali na leo itacheza mechi ya kusaka mshindi wa tatu dhidi ya Coastal Union.
Mechi ya Yanga na Azam itapigwa kuanzia saa 1:00 usiku wakati Simba na Coastal Union zitavaana kuanzia saa 9:00 alasiri kusaka mshindi wa tatu wa michuano hiyo. Endelea nayo…!
Kama hujui pambano la leo ni la tano kwa timu hizo kukutana katika michuano ya Ngao ya Jamii tangu iliposisiwa mwaka 2001.
Katika mechi nne za awali ilizokutana, Yanga imeshinda mara tatu na Azam ilishinda mara moja kwa mikwaju ya penalti miaka minane iliyopita.
Rekodi zinaonyesha kwamba timu hizo zilikutana kwa mara nne mfululizo katika mechi za Ngao, ya kwanza ikiwa ni Agosti 13, 2013 na Yanga kushinda bao 1-0 mechi iliyopigwa Kwa Mkapa (enzi hizo Uwanja wa Taifa).
Mara ya pili ilikuwa Septemba 2014, kwenye uwanja huo huo na Yanga ikashinda mabao 3-0 yaliyowekwa kimiani na Gerson Jaja kutoka Brazili aliyefunga mawili na jingine liliwekwa na Simon Msuva na msimu uliofuata wakavaana kwa mara nyingine Agosti 23, 2025 na Yanga kushinda kwa penalti 8-7 baada ya muda wa kawaida kumalizika kwa suluhu.
Katika mechi ya nne kwa timu hizo kukutana katika Ngao ya Jamii ilikuwa Agosti 17, 2016 na dakika za kawaida ziliisha kwa sare ya mabao 2-2. Yanga ilitangulia kupata mabao ya mapema kupitia kwa Donald Ngoma aliyefunga dakika ya 20 na Amissi Tambwe aliyetupia dakika nne baadaye.
Yanga ikiamini inaenda kuizamisha Azam kwa mara ya nne mfululizo, Shomari Kapombe alifunga bao dakika 75 na katika dakika za majeruhi, nahodha John Bocco alikwamisha bao la kusawazisha timu kwenda kwenye dakika za nyongeza ambazo hata hivyo hazikuzaa bao lolote na mwishowe kupigiana penalti.
Katika hatua hiyo ya penalti Azam ilifanya kweli kwa kufunga penalti 4-1 na kulipa kisasi kwa Yanga kwa kuitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza na pekee la michuano hiyo.
Mechi ya leo ni ya kisasi kwa timu zote, Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam kwa mabao 2-1, huku nyota kadhaa wa timu hiyo kushindwa kumaliza mchezo kwa kuchezewa madhambi na wenzao wa Wanalambalamba.
Kuumia kwa wachezaji kama Yao Kouassi na Pacome Zouzoua kunaelezwa ndiko kulikoinyima Yanga nafasi ya kuivaa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa imara zaidi, licha ya kutoka suluhu nje ndani na mwisho kutolewa kwa ‘matuta’.
Ni wazi, Yanga itataka kuendeleza ubabe kwa Wanalambalamba katika mechi ya leo kulipa kisasi hicho, lakini kile cha kupoteza kwa penalti pale zilipokutana mara ya mwisho katika michuano hiyo ya Ngao.
Kwa Azam itashuka ikiwa na hasira ya kupoteza mechi iliyopita ya Kombe la Shirikisho ikiwa visiwani Zanzibar. Pambano hilo lililopita lilikuwa la tatu kwa Azam katika Kombe la Shirikuisho kupoteza mbele ya Yanga, kwani ilishafungwa msimu wa 2015-16 kwa mabao 3-1, kisha ikalala 1-0 msimu wa 2022-2023 na ndipo msimu uliopita ikakaza dakika za kawaida kwa suluhu lakini ikapasuka kwa penalti 6-5.
Hakuna ubishi pambano la Yanga na Azam huwa ni kali na lenye ushindani pengine kuliko hata lile la Simba na Yanga kwa miaka ya hivi karibuni.
Hii ni kutokana na wachezaji wa timu zote kucheza kwa presha na ushindani mkubwa na kukamiana na hata msimu uliopita katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii iliyopigwa jijini Tanga, Agosti 9, ilishuhudiwa Skudu Makudubela akitumika kwa dakika saba tu kabla ya kutolewa akiwa majeruhi kwa kuchezewa rafu mbaya na kiungo James Akaminko, licha ya Azam kupoteza kwa mabao 2-0.
Ni wazi Azam haitakubali kufa kizembe kwa mara nyingine mbele ya Yanga, lakini ule upinzani wao uliopo nje ya uwanja ya kuchukuliana wachezaji muhimu kimafia ni wazi itaendelezwa katika pambano hilo.
Msimu uliopita Azam ilianzisha mizengwe na kumchukua Feisal Salum ‘Fei Toto’ kitatanishi kabla ya kupata baraka baada ya kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeialika Yanga Ikulu na kutaka imalizane na nyota huyo na mwishowe kuibukia Azam akiibeba msimu huo ikimaliza nafasi ya pili naye akiwa mfungaji bora namba mbili nyuma ya Stephane Aziz KI.
Msimu huu Azam inaivaa Yanga ikikabiliana na nyota aliyekuwa nguzo misimu minne iliyopita eneo la ushambuliaji, Prince Dube ambaye kama ilivyokuwa katika safari ya Fei Toto kwenda Yanga, ndivyo yeye alivyoifanyia Azam kwa kuanzisha mgumo baridi akipigwa tafu na Yanga na mwisho kuachana na sasa mwamba anaendelea kuvaa jezi namba 29 akiwa Jangwani kama alivyokuwa akiivaa akiwa Chamazi.
Matokeo ya mechi za nusu fainali za Ngao ya Jamii kwa msimu huu imethibitisha tofauti ya timu za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, kwani fainali ya leo inawakutanisha wawakilishi wa nchi wa michuano hiyo.
Timu hizo mbili ndizo wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, ilihali mechi ya kusaka mshindi wa tatu inazikutanisha klabu zitakazocheza Kombe la Shirikisho Afrika kwa maana ya Simba iliyomaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara na Coastal Union iliyokuwa ya nne.
Bila ya shaka kila timu itataka kuonyesha ubabe na kudhihirisha kuwa kupata nafasi ya kucheza mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika haikuwa kwa bahati mbaya bali ni uwezo, kikubwa zaidi ni kwamba timu hizo kila moja hivi karibuni zilibeba mataji katika michuano maalumu ya kimataifa iliyochezwa nje ya nchi.
Yanga ilitwaa Kombe la Toyota lililofanyika Afrika Kusini kwa kuwafunga wenyeji wao, Kaizer Chiefs kwa mabao 4-0, huku Azam nayo ikitwaa Kombe la ChopLife 2024 ikiwa Rwanda kwa kuicharaza Rayon Sports kwa bao 1-0 licha ya kuwa wenyeji wao wa Tamasha maalumu la Rayon Sports Day Kigali.
Kama zilivyo mechi nyingine za Yanga na Azam, safari hii ile vita ya mastaa kama Aziz KI dhidi ya Fei Toto, James Akaminko dhidi ya Khalid Aucho na mastaa wengine wa timu hiyo itaendelea na kazi kubwa ipo kwa makipa Diarra Djigui wa Yanga na Mohamed Mustafa.
Makipa hao katika mechi zilizopita za timu hizo, walitunguliwa na washambuliaji Aziz KI na Clement Mzize kwa upande mmoja na Gjibril Sillah na Fei Toto kwa upande wa pili ambao wachezaji hao wote bado wapo kwenye kikosi hicho ukimtoa Dube aliyehama kambi baada ya kumtungua Diarra mechi ya awali ya ligi.
Katika mechi ya kwanza ya Ngao msimu uliopita wakati Azam ikilala 2-0 pale Mkwakwani, Aziz KI na Mzize kila mmoja alifunga bao, japo walimtungua kipa chipukizi, Zubeiry Foba, lakini zilipokutana katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Azam ikilala 3-2, Aziz Ki alipiga hat trick, huku Sillah na Dube wakifunga mabao ya kufutia machozi ya Wanalambalamba, huku kipa akiwa ni Ahamada Ali.
Ziliporudiana na Azam kushinda mabao 2-1, kipa Mustafa alikuwa langoni kama ilivyokuwa kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho na Sillah na Fei Toto ndio waliotupia mabao ya Azam, huku Mzize akifunga la kufutia machozi la Yanga mbele ya kipa huyu Msudan aliyefanya kazi kubwa katika fainali ya Kombe la Shirikisho akiokoa michomo hatari ya kina Aziz KI hadi zilipoenda kupigiana penalti ya Yanga kushinda 6-5.