Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimesema iwapo kinaeleza uongo kuhusu ubadhirifu wanaoutaja hadharani, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) iridhie kuita kampuni binafsi za kimataifa kukagua miradi wanayoitaja kuwa na walakini katika utekelezaji wake.
Kimesema katika hoja 27 zilizoibuliwa na chama hicho, hakuna hata moja imejibiwa badala yake wanakituhumu na kudai hakina sera za kunadi, lakini iwapo uchunguzi huo ukifanyika itajulikana kama ni waongo ama wakweli.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya viongozi wa Serikali na CCM kueleza kuwa kauli zinazotolewa na viongozi wa ACT hazina ukweli, bali zinalenga kuwachonganisha wananchi na Serikali yake.
Hayo yalichagizwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Muhamed kueleza kuwa tuhuma zinazatolewa na viongozi hao wa kisiasa kuwa kukwama ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pemba na baadhi ya barabara za Unguja na Pemba ni upotoshaji.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika leo Jumapili Agosti 11, 2024 katika Uwanja wa Magomeni Mkoa wa Mjini Magharibi, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema pamoja na kujitutumua, hawajajibu hoja zao.
Jussa amesema kati ya mambo takribani 27 waliyoyaeleza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano yao ya hadhara wanayoifanya, bado hayajajibiwa badala yake wanabaki kutuhumu kwamba wanachonganisha na wananchi.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na ujenzi wa hospitali za wilaya, ujenzi wa shule, masoko, mradi wa ununuzi wa boti za wizara uchumi buluu, ujenzi wa mabwawa na ujenzi wa uwanja wa Amani na ukodishwaji wa visiwa vidogo.
“Duniani mnapobishania vitu kama hivyo mnaleta wakaguzi huru wa kimataifa (IIO) na zipo kampuni duniani zinafanya kazi hiyo, kama ni uongo tangaza kukubali ije kampuni ya kimataifa ikague miradi yote 27, halafu tujue nani mkweli, nani muongo,” amesema Jussa.
Jussa amesema kazi ya chama cha upinzani ni kuisimamia Serikali iliyopo madarakani, kuwaeleza ufisadi na kuwaonyesha kutowajibika, hivyo viongozi waliopo madarakani hawana budi kukubali kukosolewa na kuwaeleza wananchi majibu sahihi.
Kuhusu chama hicho kukosa sera, Jussa amesema hawana wajibu wa kuwapangia, lini wakatangaze sera zao, “hiyo ni kazi yetu sisi, lakini tunapoibua ufisadi tunafanya kazi ya siasa ya chama cha upinzani na jukumu lao ni kuwapatia wananchi majibu kama wanayo.”
Naye Mwenyekiti wa Taifa, Othman Masoud amesema inasikitisha kuona miaka 60 ya Mapinduzi, inashangaza kuona wananchi hawapati maji ndani ya nyumba zao.
“Sisi leo ikinyesha mvua kuna nyumba zinaingia maji ndani, lakini ukiyaangalia mferejini hamna, ila tumeshindwa kuchukua maji hata ya mvua watu wakapata ndani ya nyumba zao,” amesema.
Amesema Zanzibar imekwama kiuchumi na wananchi kuendelea kuishi kwenye umaskini kutokana watawala kukosa dira na maono ya namna bora ya kuendesha nchi.
“Hawa wameshajibainisha kwamba hawawezi kuongoza nchi hii badala yake ni kujinufaisha wao binafsi,” amesisitiza Othman.
Othman amesema ni aibu Zanzibar yenye historia kubwa ya uchumi imara, biashara huru na uhusiano wa kimataifa na madola makubwa ulimwenguni, lakini imepitwa kwenye maendeleo na maisha mazuri ya watu na nchi nyingine za visiwa kama Seychelles, Mauritius na Maldives.
Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo amesema mbali na kukosa uongozi wenye dira na maono, sababu nyingine kubwa inayoikwamisha Zanzibar kupiga hatua ni kutokana na kukosa mamlaka kamili kwa nchi, huku ikiwa haina uwezo wa kusimamia wala kufanya uamuzi kwa mambo zaidi ya 41 ambayo yamedhibitiwa katika Muungano.
Othman amewataka viongozi waliopo madarakani wajibu hoja zao inavyotakiwa na si kwa maneno ya kejeli.
“Tunatakiwa tuishi kwa hoja, sio kutoa maneno yasiyofaa, na kama ni kweli mnadhamira ya kweli, jibuni hoja zetu,”amesema.