Geita. Askofu wa Jimbo Katoliki Geita, Flavian Kassala ameiomba Serikali kuhakikisha inawashirikisha viongozi wa dini katika kutathimini na kushauri kuhusu masuala ya kodi ambayo ni maumivu kwa wananchi wanyonge.
Pia ameomba Serikali kutekeleza haraka msamaha wa kodi ilioutoa kwa taasisi za kidini, kwani wao hawafanyi biashara na kwamba mfumo uliokuwepo ulisababisha maumivu kwa kutoza kodi bila kuangalia huduma wanazozitoa.
Askofu Kassala amesema hayo leo Jumapili Agosti 11, 2024 wakati akitoa salamu kwenye maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25 ya upadri wake yaliyofanyika katika Parokia ya Bikra Maria Malkia wa Amani, Mjini Geita.
Maaskofu, mapadri, watawa, wanasiasa na viongozi wa Serikali wameshiriki sherehe hiyo akiwemo mgeni maalumu, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliyemwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.
Katika salamu zake, Askofu Kassala amemweleza Dk Mwigulu kufikisha pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano anaoutoa na jitihada zake za kuongoza Taifa.
Amesema Tume ya Rais ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Masuala ya Kodi itakapoanza kazi isiwasahau kuwafikia viongozi wa dini, ili waeleze maeneo ya kodi ambayo ni maumivu kwa wananchi wanyonge.
“Tunajua Rais ametangaza tume maalumu inayoshughulikia, kuangalia masuala ya kikodi, msiache kutushirikisha na sisi tukawaeleza pale ambapo pana maumivu zaidi, hasa kwa walio wanyonge kuhusiana na suala la kikodi,” amesema Askofu Kassala.
Pia, amesema taasisi za kidini hazifanyi biashara, lakini mfumo uliokuwepo ulisababisha maumivu kwa kutoza kodi bila kuangalia huduma wanazozitoa.
Tume ambayo Askofu Kassala anaizungumzia ni ile aliyoiunda Rais Samia Julai mosi, 2024, ikiwa na wajumbe tisa wabobevu wa masuala ya kodi, akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi mstafuu, Balozi Ombeni Sefue ambaye ni Mwenyekiti.
Wajumbe wengine ni aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga ambaye pia amewahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wengine ni aliyewahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.
Pia, yumo aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Price Water House Coopers (PwC) Tanzania, Leonard Mususa, Aboubakar Mohamed Aboubakar ambaye ni mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), Balozi Mwanaidi Sinare Maajari ambaye ni mshauri wa masuala ya sheria.
Wajumbe wengine ni David Tarimo ambaye ni mtaalamu na mshauri wa masuala ya kodi ambaye pia alikuwa mkuu wa idara ya ushauri wa kodi.
Wengine ni Balozi Maimuna Tarishi, katibu mkuu mstaafu na Rished Bade ambaye ni Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha ambaye pia aliwahi kuwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Julai 29, 2024, alipokuwa akihutubia mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Rais Samia ambaye ni mwenyekiti wa baraza hilo, alisema Serikali imedhamiria kuondosha changamoto zote.
“Tutaunda kamati itakayoshirikisha wajumbe kutoka serikalini na sekta binafsi, mpitie kwa undani halafu mtuletee mapendekezo na ushauri mtakaouona unafaa kwa nchi yetu kwenda na mfumo huo wa kodi,” alisema.
Kwa mujibu wa Rais Samia, ni azma ya Serikali kujenga uhusiano mzuri na wenye manufaa na sekta binafsi, ili kuongeza mapato kupitia biashara.
Alieleza anachotaka ni kuona sekta ya umma inawezesha sekta binafsi, ikiwemo kupatikana kwa rasilimali watu wenye ujuzi.
Sambamba na hayo, mkuu huyo wa nchi alisema anafahamu uwepo wa changamoto katika maeneo mbalimbali na kwamba ataendelea kuyafanyia kazi.
Alichokisema Waziri Mwigulu
Awali, akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Dk Mwigulu amesema Serikali itaendelea kuunga mkono uhuru wa kuabudu na kushirikiana na taasisi za dini katika ujenzi wa Taifa.
Amesema kupitia hoja zilizotolewa na viongozi wa dini walipokutana na Rais Samia, imesababisha kufanywa marekebisho ya sheria ya mapato ya mwaka 2014 iliyowezesha taasisi za kidini kutambuliwa kama taasisi za hisani zisizotengeneza faida.
Amesema uamuzi huo umelenga kuzipa unafuu wa masuala ya kikodi, kwa kuwa si taasisi zinazofanya biashara na badala yake zinaisaidia Serikali, hususan kwenye sekta za afya, elimu na nyinginezo.
“Kuna maeneo ambayo taasisi za dini zinaisadia Serikali sekta kama za afya, elimu na maeneo mengine, kwa hiyo sheria ya mwaka 2014 tumeirekebisha na kuziwezesha taasisi za kidini kama taasisi za hisani zisizotengeneza faida, hivyo zitapata unafuu wa kodi ya mapato,” amesema Waziri Mwigulu.
“Vilevile tumeruhusu taasisi za kidini zinazofanya miradi ya kijamii kama shule, hospitali kupata msamaha wa ongezeko la kodi yaani VAT pale zitakapofanya shughuli hizo na zimeingia makubaliano na Serikali zitakapokuwa zinatekeleza majukumu hayo,” amesema Mwigulu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mwigulu amesema R nne za Rasi Samia zimeleta matokeo makubwa, hasa kwenye hali ya siasa ambapo maridhiano na ustahimilivu yamesaidia kulileta Taifa pamoja.
“Baba Askofu naomba muendelee kuombea hali ya aina hii iendelee hivyo kutokana na utaifa wetu, ni muhimu kuliko mgawanyiko wetu na hatuwezi kwenda hatua kubwa mbele bila kuwa na umoja,” amesema.
Amesema inawezekana tulikotoka kumekuwa na mgawanyiko, lakini kwa umri wa vyama vingi uliopo tunapaswa kuhama kwenye siasa za kutugharimu na hatupaswi kurudi kwenye mazingira hayo.
Dk Mwigulu amesema kwa kuwa vyama vya siasa vipo kikatiba na Rais Samia ameleta maridhiano, ni vema vyama vya siasa kutambua tunahitaji ushindani wa sera na falsafa zinazolenga kuendeleza Taifa badala ya sisi wenyewe kugawanyika.
“Yapo maeneo watu walikuwa wanashambuliana na wakati mwingine kugharimu maisha hayo, sio maisha tunayopaswa kuendesha siasa zetu. Hata kwenye R nyingine kwa upande wa uchumi, sekta za uzalishaji zimeleta tija,” amesema.
Ameomba viongozi wa dini kushirikiana na Serikali kukemea ukatili wa kijinsia na imani za kishirikina ambazo hazina faida kwenye jamii.
Katika mahubiri yake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Eusebius Nzigilwa amesema upadri sio jambo dogo ni wito na zawadi kutoka kwa Mungu, hivyo ni vyema kufahamu upadri ni fumbo lisiloeleweka kwa nguvu za binadamu.
Amesema utume wa upadri una changamoto nyingi zinazoweza kuwakatisha tamaa, hivyo ni wajibu wa waumini kuwaombea na kuwataka mapadri kutambua pamoja na changamoto wanazokutana nazo, Mungu yupo pamoja nao.