Askofu Mbawala apewa siku 15 kukabidhi miradi kwa waasisi

Songea. Mahakama Kuu Kanda ya Songea imeliamuru Baraza la Wadhamini la Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi na Askofu Noel Mbawala, kukabidhi miradi ya uwekezaji waliyoihodhi na akaunti za benki kwa waanzilishi wa miradi hiyo.

Miradi ya uwekezaji na akaunti za benki zinazotakiwa kukabidhiwa ndani ya siku 15 ni pamoja na chuo cha ufundi, hospitali yenye chuo cha uuguzi, shule ya sekondari, uwanja wa ndege na hekari 579 vilivyopo Tunduru, Mkoa wa Ruvuma.

Amri hiyo imetolewa na Jaji James Karayemaha aliyesikiliza kesi ya madai namba 5/2022 iliyofunguliwa na Baraza la Wadhamini wa Kituo cha Elimu na Maendeleo Matemanga dhidi ya Baraza la Wadhamini wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi.

Katika kesi hiyo, Baraza la Wadhamini la Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi lilishtakiwa kama mdaiwa wa kwanza, Askofu Noel Mbawala akishtakiwa kama mdaiwa wa pili na msaidizi wake, Alphonce Manjonda kama mdaiwa wa tatu.

Jaji Karayemaha katika hukumu yake aliyoitoa Agosti 2, 2024 na nakala yake kupatikana katika mtandao wa Mahakama Agosti 11,2024, amesema miradi hiyo iligeuzwa shamba la bibi, ambapo wasiohusika walihodhi uendeshaji wake.

Vuta nikuvute ilikuwa kati ya wadai ambao ni Baraza la Wadhamini la Kituo cha Elimu na Maendeleo Matemanga na menejimenti yake dhidi ya Baraza la Wadhamini Kanisa la Upendo, Askofu Mbawala na msaidizi wake, Manjonda.

Wadai katika shauri hilo walidai wao ndio waanzilishi wa miradi hiyo ya mabilioni ya shilingi, wakati wadaiwa walijitetea kuwa wadai ni walaghai na hawana masilahi na miradi hiyo kwa kuwa walijiuzulu uongozi kwa hiari yao.

Kulingana na hukumu hiyo, Mei 29, 1996 wadhamini wa mdai waliandikishwa kwa kabidhi mkuu kama wasimamizi wakuu wa shirika lisilotengeneza faida wala kuwa na wanachama na lilianzishwa na Dk Matomora Matomora.

Baadaye mwaka 1999, shirika hilo lilisajiliwa chini ya sheria ya asasi za kiraia ambapo waanzilishi wake wakaona ni vyema waanzishe Matemanga Educational and Development Centre, ili kutoa huduma kwa jamii inayowazunguka.

Malengo ya kituo hicho ni kuondoa umaskini na hali ngumu ya maisha na kutoa huduma za matibabu kwa jamii ya vijiji vya tarafa za Matemanga na Nampungu katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Tangu kuanzishwa kwake, Dk Matomora na mkewe Ann Matomora walitambuliwa kama wamiliki, waanzilishi na wanachama wa baraza la wadhamini wa kituo hicho ambacho baadaye kilianzisha miradi ya uwekezaji.

Wakati Dk Matomora alifanya kazi kama mkurugenzi mkuu na mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa kituo hicho, mkewe Ann ambaye naye ni mwanzilishi alifanya kazi kama mkurugenzi wa fedha na utawala.

Wadai katika shauri hilo walieleza kuwa waliendelea kufurahia uhusiano mzuri na kupata ushirikiano kutoka kwa jamii iliyowazunguka na kupata misaada ya fedha kutoka ndani na nje ya nchi, iliyowasaidia kutekeleza malengo ya taasisi hiyo.

Ni kutokana na uongozi mzuri, mdai alifanikiwa kuanzisha vitega uchumi mbalimbali, kikiwamo Chuo cha Ufundi Stadi (VTC), hospitali, Matemanga Airstrip (uwanja wa ndege), kampuni ya ujenzi na kununua shamba lenye ukubwa wa ekari 579.

Mwaka 2006, Dk Matomora na mkewe Ann walianzisha Kanisa la Upendo wa Kristo na Dk Matomora aliteuliwa kuwa mdhamini na mwenyekiti, huku mkewe kuwa Katibu kwani wakati huo kanisa halikuwa na askofu.

Mwaka 2014 mdai akaanzisha chuo cha walimu kilichosajiliwa Julai 28, 2014 na shule ya mafunzo ya uuguzi iliyosajiliwa Mei 29, 2015.

Mei 2021, Dk Matomora na mkewe wakiwa ni waanzilishi na viongozi wa taasisi hizo, walilazimishwa kujiuzulu uongozi wa kanisa na kutakiwa kuondoka Tunduru na kubakia kiongozi mmoja aliyetajwa kuwa ni Joseph Mtuma.

Hata hivyo, baadaye Mtuma ambaye sasa ni marehemu naye alifukuzwa ambapo Dk Matomora, mkewe na Joseph Mtuma walipojaribu kurudi ili mgogoro huo usuluhishwe kwa njia ya amani, hawakuruhusiwa kurejea kwenye taasisi hiyo.

Mdai katika shauri hilo alidai mdaiwa wa pili na wa tatu walijitwalia uongozi kinyume cha sheria kwenye uongozi wa juu wa taasisi na walijifanya viziwi na kutosikiliza hoja yoyote ya kutaka suala hilo lisuluhishwe kwa njia za amani.

Katika utetezi wako, Askofu Mbawala na wenzake walidai tangu kuanzishwa kwa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi mwaka 2006, hospitali, VTC, sekondari, uwanja wa ndege na upatikanaji wa shamba hekari 579, vilimilikiwa na kanisa hilo.

Wakaeleza kuwa Kituo cha Elimu na Maendeleo Matemanga ni taasisi ambayo haipo (non-existing entity) na wadai katika shauri hilo ni walaghai tu, na kwamba Dk Matomora na mkewe Ann Matomora walijiuzulu kwa hiyari nafasi zote za uongozi.

Alichokisema Jaji Karayemaha

Kulingana na Jaji Karayemaha, alisema baada ya kupitia mawasilisho ya pande mbili katika mgogoro huo na vielelezo vya nyaraka zilizopokelewa kama kielelezo, wadai walisajiliwa Mei 1996 kama kituo cha Elimu na Maendeleo Matemanga.

Kuhusu hoja kama mali ni za wadai katika shauri hilo, Jaji alisema ushahidi unaonyesha wazi kuwa miradi hiyo ya uwekezaji ilianzishwa na kusajiliwa kwa jina la wadai kabla ya kuiunganisha na Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi.

Jaji alifafanua kuwa baada ya kupitia nyaraka hizo, ameona chuo cha ufundi kilisajiliwa Novemba 26, 2018 na kuendeshwa na mdai na Hospitali ya Jamii (Community Hospital) ikasajiliwa Agosti 26,2000 ikimilikiwa na wadai pia.

Shule ya sekondari nayo ilisajiliwa Julai 13,2004 ikimilikiwa na mdai, leseni ya kiwanja cha ndege iliyotolewa Mei 15,1998 ilimilikiwa na kuendeshwa na mdai na hata nyaraka zote za upatikanaji wa shamba zinamtaja mdai ndio mmiliki.

Jaji alisema hakuna ubishi kuwa walioanzisha kituo hicho ndio walioanzisha pia miradi ya uwekezaji; na akasema ni bodi ya wadhamini pekee ya wadai ndio walikuwa na haki ya kisheria kuhamisha umiliki wa mali na si mtu mwingine.

Kutokana na hayo, Jaji alitupilia mbali hoja za Askofu Mbawala na wadaiwa wengine ya kwanini wadai hawakuwashtaki waliowalazimisha kujiuzulu, akisema hoja ni nani alichukua uongozi baada ya kujiuzulu na kama kulikuwa na makabidhiano.

Jaji alisema kutokana na kutokuwepo kwa makabidhiano rasmi, miradi hiyo iligeuzwa shamba la bibi ambapo watu wasioidhinishwa walijichukulia mamlaka ya kuendesha na kusimamia miradi na kuwaweka pembeni waanzilishi.

Kwa mujibu wa Jaji, kitendo cha Askofu na wenzake kuhodhi mali hizo ilikuwa kinyume cha sheria, hivyo wanaamriwa kuwapa wadai na menejimenti yao akiwamo Dk Matomora na mkewe, haki ya kuingia ofisini na kuendelea na majukumu yao.

Jaji alisema Askofu Mbawala na wadaiwa wenzake wanaamriwa ndani ya siku 15 kuanzia tarehe ya hukumu, kukabidhi mali hizo ambazo ni shamba hekari 579, chuo cha ufundi, hospitali, shule ya sekondari na uwanja wa ndege na akaunti za benki.

Related Posts