Chato. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema hakuna namna bora ya kumuenzi Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli zaidi ya kuendeleza kazi aliyoianzisha.
Dk Nchimbi ameeleza hayo leo Jumapili, Agosti 11, 2024 baada ya kuwasili Wilaya ya Chato mkoani Geita akitokea Kagera, ikiwa ni mwanzo wa ziara yake mkoani humo.
Akiwa mkaoni humo atafanya mikutano ya hadhara na kusikiliza kero za wananchi.
Dk Nchimbi na wajumbe wa sekretarieti ya CCM wametembelea kaburi la hayati Magufuli na kuweka mashada ya maua na kushiriki ibada fupi ya kumwombea kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 17, 2021, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya ibada hiyo fupi, Dk Nchimbi amesema wajumbe wa sekretarieti wameamua kutembelea kaburi la hayati Magufuli kama ishara ya kutambua kazi kubwa aliyoifanya ndani ya Taifa na chama.
“Hayati Magufuli alipofariki aliacha miradi mingi ya maendeleo. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza miradi yote aliyoiasisi mtangulizi wake.”
“Huko aliko hayati Magufuli anaona kazi kubwa aliyoianzisha inaendelezwa,” amesema Dk Nchimbi.
Awali, akipokelewa na wananchi katika kata ya Muganza, Dk Nchimbi amesisitiza namna bora ya kumuenzi kiongozi huyo ni kuendeleza kazi kubwa aliyoianzisha katika kuwaletea wananchi maendeleo.
“Rais Samia alipoingia madarakani aliahidi kwamba hakuna mradi hata mmoja utakaosimama, sote tunaona miradi yote ikitekelezwa kikamilifu. Hii ndiyo maana ya ‘Kazi Iendelee’.
“Hakutakuwepo namna bora ya kumuenzi Rais Magufuli zaidi ya kuendeleza kazi aliyoianzisha. Rais Samia ametekeleza hilo vizuri sana,” amesema Dk Nchimbi huku akishangiliwa na wananchi wa Muganza.
Amewataka wananchi wa Chato na Mkoa wa Geita kwa ujumla kuchapa kazi kama njia ya kumuenzi hayati Magufuli ambaye alikuwa mzaliwa wa Chato.
Mbunge wa Chato (CCM), Dk Medard Kalemani amemwomba Katibu Mkuu kufikisha salamu za wananchi wa Chato kwa Rais Samia kutokana na upendo ambao amekuwa akiwaonyesha kwani ametembelea Mkoa wa Geita mara sita tangu alipoapishwa kuwa Rais, Machi 19, 2021.
Hata hivyo, ameeleza changamoto za wananchi wake kuwa ni pamoja na kukosekana kwa soko Muganza. Amesema tayari wamepata eneo kwa ajili ya kujenga soko hilo, hivyo wanaomba kupatiwa fedha ili kuanza ujenzi huo.
“Tulipata changamoto ya kituo cha Polisi, kilichokuwepo kilichomwa moto, lakini tumepata eneo jingine la kujenga kituo kingine kipya. Tunahitaji fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo,” amesema Kalemani.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amewataka wananchi wa Geita kujenga imani na chama hicho kwa sababu kinashughulika na matatizo yao na tangu Dk Nchimbi ameanza ziara zake, zaidi ya kero 1,200 zimesikilizwa na kupatiwa ufumbuzi.
“Msidanganyike na vyama vingine, CCM ndiyo chama pekee kinachoweza kutatua kero zenu. Endeleeni kujenga imani na Chama Cha Mapinduzi, kitaendelea kuisimamia Serikali ili iwaletee maendeleo,” amesema Makalla.